Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 1:1-10

1 Wafalme 1:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme Daudi, wakati alipokuwa mzee sana, watumishi wake walimfunika kwa mablanketi, lakini hata hivyo, hakuweza kupata joto. Kwa hivyo wakamwambia, “Bwana wetu mfalme, afadhali tukutafutie msichana akutumikie na kukutunza; alale pamoja nawe kusudi akupatie joto.” Basi, wakatafutatafuta msichana mzuri kote nchini Israeli. Akapatikana msichana mmoja mzuri aitwaye Abishagi, Mshunami; wakamleta kwa mfalme. Msichana huyo, alikuwa mzuri sana. Basi, akaanza kumtumikia na kumtunza mfalme; lakini mfalme hakulala naye. Wakati huo, Adoniya, mwana wa Daudi na Hagithi, akaanza kujigamba kwamba yeye ndiye atakayekuwa mfalme. Basi, akajitayarishia magari ya kukokotwa, wapandafarasi na wapiga mbio hamsini wa kumtangulia na kumshangilia. Lakini baba yake, Daudi, hakuwa amemkemea mwanawe hata mara moja na kumwuliza kwa nini alikuwa amefanya hivyo. Adoniya, ama kwa hakika, alikuwa mwenye sura ya kupendeza sana; na alikuwa amemfuata Absalomu kwa kuzaliwa. Adoniya akashauriana na Yoabu mwana wa Seruya, na kuhani Abiathari; nao wakamfuata na kumuunga mkono. Lakini kuhani Sadoki, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na nabii Nathani na Shimei, Rei pamoja na walinzi wa Daudi, hawakumuunga mkono Adoniya. Siku moja, Adoniya alitoa sadaka ya kondoo, ng'ombe na ndama wanono kwenye Jiwe la Nyoka, karibu na chemchemi iitwayo Enrogeli. Akawaalika kwenye karamu ya sadaka hiyo ndugu zake wote, yaani wana wengine wa mfalme, na watumishi wote wa mfalme waliokuwa wa kabila la Yuda. Lakini, nabii Nathani, Benaya, walinzi wa mfalme na Solomoni ndugu yake hakuwaalika.