1 Wafalme 1:1-10
1 Wafalme 1:1-10 NEN
Mfalme Daudi alipokuwa mzee umri ukiwa umesogea, hakuweza kupata joto hata walipomfunika kwa nguo. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, “Turuhusu tumtafute kijana mwanamwali bikira amhudumie mfalme na kumtunza. Anaweza kulala pembeni mwake ili bwana wetu mfalme apate joto.” Kisha wakatafuta katika Israeli yote ili kumpata msichana mzuri wa sura na wakampata Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme. Msichana huyo alikuwa mzuri sana wa sura, akamtunza mfalme na kumhudumia, lakini mfalme hakufanya naye tendo la ndoa. Basi Adoniya, ambaye mama yake alikuwa Hagithi, akajigamba na kusema, “Mimi nitakuwa mfalme.” Hivyo akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, pamoja na watu hamsini wa kumtangulia wakikimbia. (Baba yake hakuwa ameingilia na kumuuliza, “Kwa nini unafanya hivyo?” Alikuwa pia kijana mzuri sana wa sura, na alizaliwa baada ya Absalomu.) Adoniya akashauriana pamoja na Yoabu mwana wa Seruya na kuhani Abiathari, nao wakamsaidia. Lakini kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada, Nathani nabii, Shimei, Rei na walinzi maalum wa Daudi hawakujiunga na Adoniya. Ndipo Adoniya akatoa dhabihu ya kondoo, ngʼombe na ndama walionona kwenye Jiwe la Zohelethi karibu na En-Rogeli. Akawaalika ndugu zake wote, wana wa mfalme na wanaume wote wa Yuda waliokuwa maafisa wa mfalme, lakini hakumwalika nabii Nathani, Benaya, walinzi maalum wa mfalme, wala ndugu yake Solomoni.