Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 18:1-17

1 Mambo ya Nyakati 18:1-17 SRUV

Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda, akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa Wafilisti. Akapiga Moabu; na hao Wamoabi wakawa watumishi wa Daudi wakaleta zawadi. Tena Daudi akampiga Hadadezeri, mfalme wa Soba, mpaka Hamathi, alipokwenda kujisimamishia mnara wa ukumbusho kwenye mto wa Frati. Daudi akampokonya magari elfu moja, na wapanda farasi elfu saba, na askari waendao kwa miguu elfu ishirini; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila wa magari mia moja akawaweka. Na Washami wa Dameski walipokuja wamsaidie Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akapiga katika hao Washami watu elfu ishirini na mbili. Ndipo Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski; nao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda. Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumishi wa Hadadezeri akazileta Yerusalemu. Tena toka Tibhathi, na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno, aliyoitumia Sulemani katika kutengeneza lile birika la shaba, na zile nguzo, na vile vyombo vya shaba. Hata aliposikia Tou, mfalme wa Hamathi, ya kuwa Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri, mfalme wa Soba, akamtuma mwanawe Hadoramu kwa mfalme Daudi, ili kumsalimia, na kumbarikia, kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou; naye akaleta vyombo vya dhahabu, na fedha, na shaba, vya namna zote. Hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa BWANA, pamoja na hiyo fedha na dhahabu, aliyoteka nyara kwa mataifa yote; kwa Edomu, na kwa Moabu, na kwa wana wa Amoni, na kwa Wafilisti, na kwa Amaleki. Tena Abishai, mwana wa Seruya, akawaua Waedomi elfu kumi na nane katika Bonde la Chumvi. Akaweka ngome katika Edomu; na Waedomi wote wakawa watumishi wa Daudi. Naye BWANA akampa Daudi ushindi, kila alikokwenda. Basi Daudi akawatawala Waisraeli wote; akawafanyia hukumu na haki watu wake wote. Na Yoabu mwana wa Seruya akawa mkuu wa jeshi; na Yehoshafati mwana wa Ahiludi mwenye kuandika tarehe. Na Sadoki mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki mwana wa Abiathari, walikuwa makuhani; na Shausha mwandishi; na Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mkuu wa Wakerethi na Wapelethi; na wana wa Daudi walikuwa mofisa wakuu wa mfalme.