Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 18:1-17

1 Mambo ya Nyakati 18:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya hayo, mfalme Daudi aliwashinda na kuwatiisha Wafilisti. Akauteka mji wa Gathi pamoja na vijiji vyake walivyomiliki Wafilisti. Aliwashinda Wamoabu pia, wakawa watumishi wake na wakawa wanalipa kodi. Daudi pia alimshinda Hadadezeri mfalme wa Soba, nchi iliyokuwa karibu na Hamathi, alifanya hivyo wakati alipokuwa akienda kujisimamishia nguzo ya kumbukumbu kwenye sehemu za mto Eufrate. Daudi akateka magari ya farasi 1,000, askari wapandafarasi 7,000 na wa miguu 20,000. Kisha Daudi alikata mishipa ya miguu ya nyuma ya farasi wote wa magari, ila aliwabakiza 100. Nao Waaramu wa Damasko, walipokwenda kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi aliwashambulia na kuwaua watu 22,000. Halafu Daudi aliweka kambi za kijeshi katika mji wa Shamu ya Damasko. Basi Waaramu wakawa watumishi wake, na wakawa wanalipa kodi. Mwenyezi-Mungu alimpa Daudi ushindi kokote alikokwenda. Daudi alizichukua ngao za dhahabu walizobeba wanajeshi wa Hadadezeri, na kuzipeleka Yerusalemu. Daudi alichukua pia shaba nyingi sana kutoka mji wa Tibhathi na mji wa Kuni; iliyokuwa miji ya Hadadezeri. Solomoni aliitumia shaba hiyo kutengenezea nguzo na vyombo vya shaba. Wakati Tou, mfalme wa Hamathi aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri mfalme wa Soba, alituma mwanawe Hadoramu kwa mfalme Daudi, kumpelekea salamu na pongezi kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri na kumshinda. Maana Hadadezeri alipigana na Tou mara nyingi. Hadoramu alimpelekea Daudi zawadi za vyombo vya fedha, dhahabu na shaba. Zawadi hizo, mfalme Daudi aliziweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu pamoja na fedha na dhahabu aliyoiteka kutoka mataifa yote kutoka: Edomu, Moabu, Amoni, Filisti na Amaleki. Abishai mwana wa Seruya, aliwaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi. Basi akaweka kambi za kijeshi huko Edomu. Nao Waedomu wote wakawa watumishi wa Daudi. Mwenyezi-Mungu alimpa Daudi ushindi kokote alikokwenda. Hivyo Daudi akatawala juu ya Israeli yote, na akahakikisha ya kwamba watu wake wote wanatendewa haki na usawa. Yoabu, mwana wa Seruya alikuwa mkuu wa majeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mtunza kumbukumbu; Sadoki, mwana wa Ahitubu na Ahimeleki, mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Shausha alikuwa katibu; na Benaya, mwana wa Yehoyada alisimamia askari walinzi Wakerethi na Wapelethi; wana wa Daudi walikuwa maofisa wakuu katika utawala wake.

1 Mambo ya Nyakati 18:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda, akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa Wafilisti. Akapiga Moabu; na hao Wamoabi wakawa watumishi wa Daudi wakaleta zawadi. Tena Daudi akampiga Hadadezeri, mfalme wa Soba, mpaka Hamathi, alipokwenda kujisimamishia mnara wa ukumbusho kwenye mto wa Frati. Daudi akampokonya magari elfu moja, na wapanda farasi elfu saba, na askari waendao kwa miguu elfu ishirini; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila wa magari mia moja akawaweka. Na Washami wa Dameski walipokuja wamsaidie Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akapiga katika hao Washami watu elfu ishirini na mbili. Ndipo Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski; nao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda. Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumishi wa Hadadezeri akazileta Yerusalemu. Tena toka Tibhathi, na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno, aliyoitumia Sulemani katika kutengeneza lile birika la shaba, na zile nguzo, na vile vyombo vya shaba. Hata aliposikia Tou, mfalme wa Hamathi, ya kuwa Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri, mfalme wa Soba, akamtuma mwanawe Hadoramu kwa mfalme Daudi, ili kumsalimia, na kumbarikia, kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou; naye akaleta vyombo vya dhahabu, na fedha, na shaba, vya namna zote. Hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa BWANA, pamoja na hiyo fedha na dhahabu, aliyoteka nyara kwa mataifa yote; kwa Edomu, na kwa Moabu, na kwa wana wa Amoni, na kwa Wafilisti, na kwa Amaleki. Tena Abishai, mwana wa Seruya, akawaua Waedomi elfu kumi na nane katika Bonde la Chumvi. Akaweka ngome katika Edomu; na Waedomi wote wakawa watumishi wa Daudi. Naye BWANA akampa Daudi ushindi, kila alikokwenda. Basi Daudi akawatawala Waisraeli wote; akawafanyia hukumu na haki watu wake wote. Na Yoabu mwana wa Seruya akawa mkuu wa jeshi; na Yehoshafati mwana wa Ahiludi mwenye kuandika tarehe. Na Sadoki mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki mwana wa Abiathari, walikuwa makuhani; na Shausha mwandishi; na Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mkuu wa Wakerethi na Wapelethi; na wana wa Daudi walikuwa mofisa wakuu wa mfalme.

1 Mambo ya Nyakati 18:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda, akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa Wafilisti. Akapiga Moabu; na hao Wamoabi wakawa watumwa wa Daudi wakaleta zawadi. Tena Daudi akampiga Hadadezeri, mfalme wa Soba, mpaka Hamathi, alipokwenda kujisimamishia mamlaka yake kwenye mto wa Frati. Daudi akampokonya magari elfu, na wapanda farasi saba elfu, na askari waendao kwa miguu ishirini elfu; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila wa magari mia akawaweka. Na Washami wa Dameski walipokuja wamsaidie Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akapiga katika hao Washami watu ishirini na mbili elfu. Ndipo Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski; nao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda. Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumishi wa Hadadezeri akazileta Yerusalemu. Tena toka Tibhathi, na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno, aliyofanyizia Sulemani ile bahari ya shaba, na zile nguzo, na vile vyombo vya shaba. Hata aliposikia Tou, mfalme wa Hamathi, ya kuwa Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri, mfalme wa Soba, akampeleka mwanawe Hadoramu kwa mfalme Daudi, ili kumsalimia, na kumbarikia, kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou; naye akaleta vyombo vya dhahabu, na fedha, na shaba, vya namna zote. Hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa BWANA, pamoja na hiyo fedha na dhahabu, aliyoteka nyara kwa mataifa yote; kwa Edomu, na kwa Moabu, na kwa wana wa Amoni, na kwa Wafilisti, na kwa Amaleki. Tena Abishai, mwana wa Seruya, akawapiga wa Waedomi katika Bonde la Chumvi watu kumi na nane elfu. Akaweka ngome katika Edomu; na Waedomi wote wakawa watumwa wa Daudi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda, kila alikokwenda. Basi Daudi akatawala juu ya Israeli wote; akawafanyia hukumu na haki watu wake wote. Na Yoabu mwana wa Seruya akawa juu ya jeshi; na Yehoshafati mwana wa Ahiludi mwenye kuandika tarehe. Na Sadoki mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki mwana wa Abiathari, walikuwa makuhani; na Shausha mwandishi; na Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi; na wana wa Daudi walikuwa wakuu kumzunguka mfalme.

1 Mambo ya Nyakati 18:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akautwaa Gathi pamoja na vijiji vinavyouzunguka kutoka utawala wa Wafilisti. Pia Daudi akawashinda Wamoabu, wakawa watumishi wake, nao wakawa wanamletea ushuru. Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mfalme wa Soba, hadi Hamathi, wakati alikwenda kuimarisha utawala wake katika Mto Frati. Daudi akateka magari ya vita 1,000 miongoni mwa magari yake, waendesha hayo magari ya kukokotwa na farasi 7,000 na askari wa miguu 20,000. Daudi akakata mishipa ya miguu ya nyuma ya farasi wote wakokotao magari, ila akabakiza 100. Waaramu wa Dameski, walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua 22,000 miongoni mwao. Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski. Basi Waaramu wakawa watumwa wa Daudi, na kumlipa ushuru. BWANA akampa Daudi ushindi kote alipokwenda. Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu. Kutoka miji ya Tibhathi na Kuni, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi sana, ambayo Solomoni aliitumia kutengenezea ile Bahari ya shaba, zile nguzo na vifaa mbalimbali vya shaba. Tou mfalme wa Hamathi aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri mfalme wa Soba, akamtuma mwanawe, Hadoramu kwa Mfalme Daudi ili kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Mfalme Hadadezeri, kwa kuwa alikuwa amepigana vita mara nyingi na Tou. Hadoramu akamletea Daudi vifaa mbalimbali vya dhahabu, fedha na shaba. Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa BWANA kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu aliyokuwa ameitwaa katika mataifa yote haya: Edomu na Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki. Abishai mwana wa Seruya akawaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi. Akaweka kambi za askari walinzi huko Edomu, nao Waedomu wote wakawa watumishi wa Daudi. BWANA akampa Daudi ushindi kila alipokwenda. Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote. Yoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu; Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Shausha alikuwa mwandishi; naye Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa maafisa wakuu katika utumishi wa mfalme.