Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 12:1-40

1 Mambo ya Nyakati 12:1-40 SRUV

Basi hawa ndio wale waliomjia Daudi huko Siklagi, alipokuwa akijificha kwa ajili ya Sauli, mwana wa Kishi; nao walikuwamo miongoni mwa wale mashujaa, waliomsaidia vitani. Walikuwa wenye kupinda upinde, nao walikuwa hodari wa kutumia mkono wa kulia na wa kushoto, kwa kutupa mawe ya teo, na kwa kupiga mishale ya upinde; walikuwa wa nduguze Sauli, wa Benyamini. Mkubwa wao alikuwa Ahiezeri, kisha Yoashi, wana wa Shemaa Mgibeathi; na Yezieli, na Peleti, wana wa Azmawethi; na Beraka, na Yehu Mwanathothi; na Ishmaya Mgibeoni, shujaa wa wale thelathini, naye alikuwa juu ya wale thelathini; na Yeremia, na Yahazieli, na Yohana, na Yozabadi Mgederathi; Eluzai, na Yerimothi, na Bealia, na Shemaria, na Shefatia Mharufi; Elkana, na Ishia, na Azaleli, na Yoezeri, na Yashobeamu, Wakora; na Yoela, na Zebadia, wana wa Yerohamu, wa Gedori. Na wa Wagadi wakajitenga kumfuata Daudi ngomeni huko nyikani, wanaume mashujaa, watu waliozoea vita, walioweza kutumia ngao na mkuki; ambao nyuso zao zilikuwa kama nyuso za simba, nao walikuwa wepesi kama kulungu juu ya milima; Ezeri mkubwa wao, Obadia wa pili, Eliabu wa tatu; Mishmana wa nne, Yeremia wa tano; Atai wa sita, Elieli wa saba; Yohana wa nane, Elzabadi wa tisa; Yeremia wa kumi, Makbanai wa kumi na moja. Hao Wagadi walikuwa makamanda wa jeshi, yeye aliyekuwa mdogo amelingana na mia moja, na yeye aliyekuwa mkuu, na elfu moja. Hao ndio wale waliovuka Yordani katika mwezi wa kwanza, ulipofurika kingo zake zote; nao wakawakimbiza wote wa bondeni kuelekea mashariki na magharibi pia. Tena wakafika ngomeni kwa Daudi baadhi ya wana wa Benyamini na Yuda. Naye Daudi akatoka ili kuwalaki, akajibu, akawaambia, Kama mmenijia kwa amani ili kunisaidia, basi nitawapokea kwa moyo wote; lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa adui zangu, ingawa hamna udhalimu mikononi mwangu, Mungu wa baba zetu na alitazame neno hili, na kulikemea. Ndipo roho ikamjia Abishai, mkuu wa wale thelathini, naye akasema, Sisi tu watu wako, Ee Daudi; Na wa upande wako, Ee mwana wa Yese; Amani, naam, amani iwe kwako, Na amani iwe kwao wakusaidiao; Maana Mungu wako ndiye akusaidiye. Ndipo Daudi akawakaribisha, akawaweka wawe makamanda wa kile kikosi. Baadhi ya wana wa Manase walimwangukia Daudi, alipokwenda pamoja na Wafilisti juu ya Sauli vitani, lakini hawakuwasaidia; kwani wale mabwana wa Wafilisti wakafanya shauri, wakamfukuza, wakisema, tunahatarisha maisha yetu maana atamwangukia bwana wake Sauli. Naye alipokuwa akienda Siklagi, Manase hawa wakamwangukia, Adna, na Yozabadi, na Yediaeli, na Mikaeli, na Yozabadi, na Elihu, na Silethai, makamanda wa maelfu waliokuwa wa Manase. Wakamsaidia Daudi juu ya kile kikosi kilichomshambulia; kwani walikuwa wanaume mashujaa wote, nao wakawa makamanda jeshini. Maana siku baada ya siku watu waliomwendea Daudi ili kumsaidia, hadi wakapata kuwa jeshi kubwa, kama jeshi la Mungu. Na hizi ni hesabu za vichwa vya watu wenye silaha za vita, waliokuja Hebroni kwa Daudi, ili kumpa ufalme wa Sauli, sawasawa na neno la BWANA. Wana wa Yuda, waliochukua ngao na mkuki, walikuwa elfu sita na mia nane, wenye silaha za vita. Wa wana wa Simeoni, wanaume mashujaa wa vita, elfu saba na mia moja. Wa wana wa Lawi, elfu nne na mia sita. Na Yehoyada alikuwa kichwa cha ukoo wa Haruni, na pamoja naye walikuwa watu elfu tatu na mia saba; tena Sadoki, kijana shujaa, na wa nyumba ya babaye, makamanda ishirini na wawili. Na wa wana wa Benyamini nduguze Sauli, elfu tatu; kwani hata sasa walio wengi wao walikuwa wameuhifadhi uaminifu wao kwa nyumba ya Sauli. Na wa wana wa Efraimu, elfu ishirini na mia nane, wanaume mashujaa, watu wenye sifa katika koo za baba zao. Na wa nusu kabila la Manase, elfu kumi na nane, waliotajwa majina yao, ili waje kumtawaza Daudi awe mfalme. Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao. Wa Zabuloni, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, wenye zana za vita za kila namna, elfu hamsini; askari stadi waliolenga tu kumsaidia Daudi. Na wa Naftali, makamanda elfu moja, na pamoja nao watu wenye ngao na mkuki elfu thelathini na saba. Na wa Wadani, watu hodari wa kupanga vita, elfu ishirini na nane na mia sita. Na wa Asheri, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, elfu arubaini. Tena, ng'ambo ya pili ya Yordani, wa Wareubeni, na wa Wagadi, na wa nusu kabila la Manase, wenye zana za vita za kupigania za kila namna, elfu mia moja na ishirini. Hao wote, watu wa vita, askari stadi, wakaja Hebroni wakiwa na nia moja ya kumtawaza Daudi awe mfalme juu ya Israeli wote; tena wote waliosalia wa Israeli nao walikuwa na moyo mmoja kwamba wamtawaze Daudi. Nao walikuwako huko pamoja na Daudi siku tatu, wakila na kunywa; kwani ndugu zao walikuwa wamewaandalia tayari. Zaidi ya hayo, wale waliokuwa karibu nao, hata mpaka kwa Isakari, na Zabuloni, na Naftali, wakaleta chakula juu ya punda, na ngamia, na nyumbu, na ng'ombe, vyakula vya unga, mikate ya tini, na vichala vya zabibu kavu, na divai, na mafuta, na ng'ombe, na kondoo tele; kwa kuwa kulikuwa na furaha katika Israeli.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha