Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 12:1-40

1 Mambo ya Nyakati 12:1-40 Biblia Habari Njema (BHN)

Hawa ni wanaume ambao walijiunga na Daudi huko Siklagi, alipokuwa hana uhuru wowote wa kutembea kwa sababu ya mfalme Shauli mwana wa Kishi; walikuwa miongoni mwa askari mashujaa waliomsaidia vitani. Hao walikuwa watu wa kabila la Benyamini kama alivyokuwa Shauli. Walikuwa wapiga upinde hodari, na warusha mawe kwa kombeo kwa kutumia mikono yote, wa kulia na kushoto. Kiongozi wao alikuwa Ahiezeri, aliyesaidiwa na Yoashi, wote wana wa Shemaa kutoka Gibea; wengineo ni: Yezieli na Peleti, wana wa Azmawethi, Beraka, Yehu kutoka Anathothi, Ishmaya kutoka Gibeoni, mtu shujaa miongoni mwa wale thelathini na kiongozi wao pia pamoja na Yeremia, Yahazieli, Yohanani, Yozabadi kutoka Gedera, Eluzai, Yeremothi, Bealia, Shemaria, Shefatia, Mharufi, Elkana, Ishia, Azareli, Yoezeri, Yashobeamu kutoka ukoo wa Kora na Yoela na Zebadia, wana wa Yerohamu, kutoka Gedori. Tena, watu kutoka kabila la Gadi walijiunga na Daudi akiwa ngomeni kule nyikani. Hawa walikuwa askari wenye nguvu na uzoefu, hodari wa kutumia ngao na mkuki; wenye nyuso za kutisha kama simba na wepesi kama swala milimani. Kiongozi wao mkuu alikuwa Ezeri, wa pili Obadia, wa tatu Eliabu, wa nne Mishmana, wa tano Yeremia, wa sita Atai, wa saba Elieli, wa nane Yohanani, wa tisa Elsabadi, wa kumi Yeremia, na wa kumi na moja Makbanai. Wagadi hao, walikuwa maofisa wa jeshi. Kulingana na vyeo vyao, mdogo alisimamia kikosi cha wanajeshi 100, na mkubwa alisimamia kikosi cha wanajeshi 1,000. Hawa ndio watu waliovuka mto Yordani mnamo mwezi wa kwanza, mto ulipokuwa umefurika pande zote na kuwatawanya watu mashariki na magharibi ya mto. Baadhi ya watu kutoka makabila ya Benyamini na Yuda walifika ngomeni alipokuwa Daudi. Daudi akatoka nje kuwalaki, akawaambia, “Ikiwa mmekuja kwangu kama marafiki ili kunisaidia basi nawapokea kwa moyo wote, lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa maadui zangu, ingawa sijatenda ovu lolote, Mungu wa baba zetu awaone na awakemee.” Hapo Roho akamjia Abishai, mkuu wa hao watu thelathini, naye akasema, “Sisi tu watu wako, ee Daudi, tuko upande wako, ee mwana wa Yese! Amani, amani iwe kwako, na amani iwe kwa yeyote akusaidiaye! Maana akusaidiaye ndiye Mungu wako.” Ndipo Daudi akawapokea na kuwafanya maofisa katika jeshi lake. Askari wengine wa kabila la Manase, walitoroka na kujiunga na Daudi, wakati alipoondoka pamoja na Wafilisti kwenda kupigana na mfalme Shauli. (Lakini hata hivyo, hakuwasaidia maana watawala wa Wafilisti walifanya shauri wamfukuze arudi Siklagi wakisema, “Tutayahatarisha maisha yetu kwa sababu atatutoroka arudi kwa bwana wake Shauli.”) Basi, Daudi alipokuwa Siklagi, watu wafuatao wa kabila la Manase walimwendea: Adna, Yozabadi, Yediaeli, Mikaeli, Yozabadi, Elihu na Silethai. Kila mmoja wao alikuwa kiongozi wa kikosi cha watu 1,000 katika kabila la Manase. Walimsaidia Daudi kupigana na magenge ya washambuliaji, kwani wote walikuwa askari mashujaa na makamanda jeshini. Siku hata siku, watu walijiunga na Daudi kumsaidia, hatimaye akawa na jeshi kubwa sana, kama jeshi la Mungu. Hii ndio idadi ya vikosi vya askari wenye silaha waliojiunga na Daudi huko Hebroni ili kumtwalia ufalme kutoka kwa Shauli, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu: Watu wa kabila la Yuda waliokuwa na mikuki na ngao, walikuwa 6,800. Wote walikuwa na silaha zao. Kutoka kabila la Simeoni, watu 7,100 mashujaa na wenye ujuzi mwingi wa vita. Kutoka kabila la Lawi: Watu 4,600. Yehoyada, wa uzao wa Aroni na wenzake: Watu 3,700. Jamaa ya Sadoki, kijana hodari vitani, yeye pamoja na makamanda ishirini na wawili kutoka ukoo wa baba yake mwenyewe. Kutoka kabila la Benyamini, (kabila la Shauli): Watu 3,000. Wengi wao walibaki waaminifu kwa jamaa ya Shauli; Kutoka kabila la Efraimu: Watu 20,800, watu mashujaa sana tena mashuhuri katika koo zao; Kutoka nusu ya kabila la Manase: Watu 18,000, waliotajwa majina ili waje kumtawaza Daudi awe mfalme. Kutoka kabila la Isakari: Wakuu 200 pamoja na ndugu zao wote waliokuwa chini ya amri yao. Wakuu hao walikuwa na elimu ya kujua mambo ya nyakati na walijua kilichowapasa Waisraeli kufanya. Kutoka kabila la Zebuluni: Watu 50,000; waaminifu na wazoefu wa vita. Walijiandaa na zana za vita za kila namna, lengo lao likiwa ni kumsaidia Daudi tu. Kutoka kabila la Naftali: Makamanda 1,000 pamoja na watu 37,000 wenye ngao na mikuki. Kutoka kabila la Dani: Watu 28,600 wenye silaha tayari kwa vita. Kutoka kabila la Asheri: Watu 40,000 wazoefu wa vita, tayari kwa mapigano. Kutoka kabila la Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kutoka ngambo ya mto Yordani: Watu 120,000 wenye kila aina ya silaha za vita. Wanajeshi hao wote, waliojiandaa tayari kabisa kwa vita, walikwenda Hebroni na nia yao kubwa ikiwa ni kumtawaza Daudi awe mfalme wa Israeli yote. Nao watu wote wa Israeli, pia waliungana wakiwa na nia moja ya kumtawaza Daudi awe mfalme. Basi, walikaa na Daudi kwa muda wa siku tatu, wakila na kunywa kwani ndugu zao walikuwa wamekwisha waandalia vyakula. Zaidi ya hayo, majirani zao wa karibu na hata wa mbali kama huko Isakari, Zebuluni na Naftali, waliwaletea vyakula walivyobeba kwa punda, ngamia, nyumbu na ng'ombe. Waliwaletea unga, mikate ya tini, vichala vya zabibu kavu, divai na mafuta, ng'ombe na kondoo wengi, kukawa na vyakula tele, kwani kulikuwa na furaha katika Israeli.

1 Mambo ya Nyakati 12:1-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi hawa ndio wale waliomjia Daudi huko Siklagi, alipokuwa akijificha kwa ajili ya Sauli, mwana wa Kishi; nao walikuwamo miongoni mwa wale mashujaa, waliomsaidia vitani. Walikuwa wenye kupinda upinde, nao walikuwa hodari wa kutumia mkono wa kulia na wa kushoto, kwa kutupa mawe ya teo, na kwa kupiga mishale ya upinde; walikuwa wa nduguze Sauli, wa Benyamini. Mkubwa wao alikuwa Ahiezeri, kisha Yoashi, wana wa Shemaa Mgibeathi; na Yezieli, na Peleti, wana wa Azmawethi; na Beraka, na Yehu Mwanathothi; na Ishmaya Mgibeoni, shujaa wa wale thelathini, naye alikuwa juu ya wale thelathini; na Yeremia, na Yahazieli, na Yohana, na Yozabadi Mgederathi; Eluzai, na Yerimothi, na Bealia, na Shemaria, na Shefatia Mharufi; Elkana, na Ishia, na Azaleli, na Yoezeri, na Yashobeamu, Wakora; na Yoela, na Zebadia, wana wa Yerohamu, wa Gedori. Na wa Wagadi wakajitenga kumfuata Daudi ngomeni huko nyikani, wanaume mashujaa, watu waliozoea vita, walioweza kutumia ngao na mkuki; ambao nyuso zao zilikuwa kama nyuso za simba, nao walikuwa wepesi kama kulungu juu ya milima; Ezeri mkubwa wao, Obadia wa pili, Eliabu wa tatu; Mishmana wa nne, Yeremia wa tano; Atai wa sita, Elieli wa saba; Yohana wa nane, Elzabadi wa tisa; Yeremia wa kumi, Makbanai wa kumi na moja. Hao Wagadi walikuwa makamanda wa jeshi, yeye aliyekuwa mdogo amelingana na mia moja, na yeye aliyekuwa mkuu, na elfu moja. Hao ndio wale waliovuka Yordani katika mwezi wa kwanza, ulipofurika kingo zake zote; nao wakawakimbiza wote wa bondeni kuelekea mashariki na magharibi pia. Tena wakafika ngomeni kwa Daudi baadhi ya wana wa Benyamini na Yuda. Naye Daudi akatoka ili kuwalaki, akajibu, akawaambia, Kama mmenijia kwa amani ili kunisaidia, basi nitawapokea kwa moyo wote; lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa adui zangu, ingawa hamna udhalimu mikononi mwangu, Mungu wa baba zetu na alitazame neno hili, na kulikemea. Ndipo roho ikamjia Abishai, mkuu wa wale thelathini, naye akasema, Sisi tu watu wako, Ee Daudi; Na wa upande wako, Ee mwana wa Yese; Amani, naam, amani iwe kwako, Na amani iwe kwao wakusaidiao; Maana Mungu wako ndiye akusaidiye. Ndipo Daudi akawakaribisha, akawaweka wawe makamanda wa kile kikosi. Baadhi ya wana wa Manase walimwangukia Daudi, alipokwenda pamoja na Wafilisti juu ya Sauli vitani, lakini hawakuwasaidia; kwani wale mabwana wa Wafilisti wakafanya shauri, wakamfukuza, wakisema, tunahatarisha maisha yetu maana atamwangukia bwana wake Sauli. Naye alipokuwa akienda Siklagi, Manase hawa wakamwangukia, Adna, na Yozabadi, na Yediaeli, na Mikaeli, na Yozabadi, na Elihu, na Silethai, makamanda wa maelfu waliokuwa wa Manase. Wakamsaidia Daudi juu ya kile kikosi kilichomshambulia; kwani walikuwa wanaume mashujaa wote, nao wakawa makamanda jeshini. Maana siku baada ya siku watu waliomwendea Daudi ili kumsaidia, hadi wakapata kuwa jeshi kubwa, kama jeshi la Mungu. Na hizi ni hesabu za vichwa vya watu wenye silaha za vita, waliokuja Hebroni kwa Daudi, ili kumpa ufalme wa Sauli, sawasawa na neno la BWANA. Wana wa Yuda, waliochukua ngao na mkuki, walikuwa elfu sita na mia nane, wenye silaha za vita. Wa wana wa Simeoni, wanaume mashujaa wa vita, elfu saba na mia moja. Wa wana wa Lawi, elfu nne na mia sita. Na Yehoyada alikuwa kichwa cha ukoo wa Haruni, na pamoja naye walikuwa watu elfu tatu na mia saba; tena Sadoki, kijana shujaa, na wa nyumba ya babaye, makamanda ishirini na wawili. Na wa wana wa Benyamini nduguze Sauli, elfu tatu; kwani hata sasa walio wengi wao walikuwa wameuhifadhi uaminifu wao kwa nyumba ya Sauli. Na wa wana wa Efraimu, elfu ishirini na mia nane, wanaume mashujaa, watu wenye sifa katika koo za baba zao. Na wa nusu kabila la Manase, elfu kumi na nane, waliotajwa majina yao, ili waje kumtawaza Daudi awe mfalme. Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao. Wa Zabuloni, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, wenye zana za vita za kila namna, elfu hamsini; askari stadi waliolenga tu kumsaidia Daudi. Na wa Naftali, makamanda elfu moja, na pamoja nao watu wenye ngao na mkuki elfu thelathini na saba. Na wa Wadani, watu hodari wa kupanga vita, elfu ishirini na nane na mia sita. Na wa Asheri, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, elfu arubaini. Tena, ng'ambo ya pili ya Yordani, wa Wareubeni, na wa Wagadi, na wa nusu kabila la Manase, wenye zana za vita za kupigania za kila namna, elfu mia moja na ishirini. Hao wote, watu wa vita, askari stadi, wakaja Hebroni wakiwa na nia moja ya kumtawaza Daudi awe mfalme juu ya Israeli wote; tena wote waliosalia wa Israeli nao walikuwa na moyo mmoja kwamba wamtawaze Daudi. Nao walikuwako huko pamoja na Daudi siku tatu, wakila na kunywa; kwani ndugu zao walikuwa wamewaandalia tayari. Zaidi ya hayo, wale waliokuwa karibu nao, hata mpaka kwa Isakari, na Zabuloni, na Naftali, wakaleta chakula juu ya punda, na ngamia, na nyumbu, na ng'ombe, vyakula vya unga, mikate ya tini, na vichala vya zabibu kavu, na divai, na mafuta, na ng'ombe, na kondoo tele; kwa kuwa kulikuwa na furaha katika Israeli.

1 Mambo ya Nyakati 12:1-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi hawa ndio wale waliomjia Daudi huko Siklagi, alipokuwa akijificha kwa ajili ya Sauli, mwana wa Kishi; nao walikuwamo miongoni mwa wale mashujaa, waliomsaidia vitani. Walikuwa wenye kupinda upinde, nao walikuwa hodari wa kutumia mkono wa kuume na wa kushoto, kwa kutupa mawe ya teo, na kwa kupiga mishale ya upinde; walikuwa wa nduguze Sauli, wa Benyamini. Mkubwa wao alikuwa Ahiezeri, kisha Yoashi, wana wa Shemaa Mgibeathi; na Yezieli, na Peleti, wana wa Azmawethi; na Beraka, na Yehu Mwanathothi; na Ishmaya Mgibeoni, shujaa wa wale thelathini, naye alikuwa juu ya wale thelathini; na Yeremia, na Yahazieli, na Yohana, na Yozabadi Mgederathi; Eluzai, na Yerimothi, na Bealia, na Shemaria, na Shefatia Mharufi; Elkana, na Ishia, na Azaleli, na Yoezeri, na Yashobeamu, Wakora; na Yoela, na Zebadia, wana wa Yerohamu, wa Gedori. Na wa Wagadi wakajitenga kumfuata Daudi ngomeni huko nyikani, waume mashujaa, watu waliozoea vita, walioweza kutumia ngao na mkuki; ambao nyuso zao zilikuwa kama nyuso za simba, nao walikuwa wepesi kama kulungu juu ya milima; Ezeri mkubwa wao, Obadia wa pili, Eliabu wa tatu; Mishmana wa nne, Yeremia wa tano; Atai wa sita, Elieli wa saba; Yohana wa nane, Elzabadi wa kenda; Yeremia wa kumi, Makbanai wa kumi na moja. Hao wa wana wa Gadi walikuwa maakida wa jeshi, yeye aliyekuwa mdogo amelingana na mia, na yeye aliyekuwa mkuu, na elfu. Hao ndio wale waliovuka Yordani katika mwezi wa kwanza, ulipofurika kingo zake zote; nao wakawakimbiza wote wa bondeni kuelekea mashariki na magharibi pia. Tena wakafika ngomeni kwa Daudi baadhi ya wana wa Benyamini na Yuda. Naye Daudi akatoka ili kuwalaki, akajibu, akawaambia, Kama mmenijia kwa amani ili kunisaidia, basi moyo wangu utaambatana nanyi; lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa adui zangu, kwa kuwa hamna udhalimu mikononi mwangu, Mungu wa baba zetu na alitazame neno hili, na kulikemea. Ndipo roho ikamjilia Abishai, mkuu wa wale thelathini, naye akasema, Sisi tu watu wako, Ee Daudi; Na wa upande wako, Ee mwana wa Yese; Amani, naam, amani iwe kwako, Na amani iwe kwao wakusaidiao; Maana akusaidiye ndiye Mungu wako. Ndipo Daudi akawakaribisha, akawaweka wawe maakida wa kile kikosi. Wa Manase pia wengine walimwangukia Daudi, alipokwenda pamoja na Wafilisti juu ya Sauli vitani, lakini hawakuwasaidia; kwani wale mabwana wa Wafilisti wakafanya shauri, wakamfukuza, wakisema, kwa hatari ya vichwa vyetu atamwangukia bwana wake Sauli. Naye alipokuwa akienda Siklagi, wakamwangukia hawa wa Manase, Adna, na Yozabadi, na Yediaeli, na Mikaeli, na Yozabadi, na Elihu, na Silethai, maakida wa maelfu waliokuwa wa Manase. Wakamsaidia Daudi juu ya kile kikosi kilichomshambulia; kwani walikuwa waume mashujaa wote, nao wakawa maakida jeshini. Maana siku kwa siku humjia Daudi watu wa kumsaidia, hata wakapata kuwa jeshi kubwa, kama jeshi la Mungu. Na hizi ni hesabu za vichwa vya watu wenye silaha za vita, waliokuja Hebroni kwa Daudi, ili kumgeuzia ufalme wa Sauli, sawasawa na neno la BWANA. Wana wa Yuda, waliochukua ngao na mkuki, walikuwa elfu sita na mia nane, wenye silaha za vita. Wa wana wa Simeoni, waume mashujaa wa vita, elfu saba na mia moja. Wa wana wa Lawi, elfu nne na mia sita. Na Yehoyada alikuwa kichwa cha mbari ya Haruni, na pamoja naye walikuwa elfu tatu na mia saba; tena Sadoki, kijana shujaa, na wa nyumba ya babaye, maakida ishirini na wawili. Na wa wana wa Benyamini nduguze Sauli, elfu tatu; kwani hata sasa walio wengi wao walikuwa wameuhifadhi uaminifu wao kwa nyumba ya Sauli. Na wa wana wa Efraimu, ishirini elfu na mia nane, waume mashujaa, watu wenye sifa katika mbari za baba zao. Na wa nusu kabila ya Manase, kumi na nane elfu, waliotajwa majina yao, ili waje kumtawaza Daudi awe mfalme. Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao. Wa Zabuloni, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, wenye zana za vita za kila namna, hamsini elfu; askari wastadi wasiokuwa wenye moyo wa kusita-sita. Na wa Naftali, maakida elfu, na pamoja nao watu wenye ngao na mkuki thelathini na saba elfu. Na wa Wadani, watu hodari wa kupanga vita, ishirini na nane elfu na mia sita. Na wa Asheri, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, arobaini elfu. Tena, ng’ambo ya pili ya Yordani, wa Wareubeni, na wa Wagadi, na wa nusu kabila ya Manase, wenye zana za vita za kupigania za kila namna, mia na ishirini elfu. Hao wote, watu wa vita, askari wastadi, wakaja Hebroni wenye moyo mkamilifu, ili kumtawaza Daudi awe mfalme juu ya Israeli wote; tena wote waliosalia wa Israeli nao walikuwa na moyo mmoja kwamba wamtawaze Daudi. Nao walikuwako huko pamoja na Daudi siku tatu, wakila na kunywa; kwani ndugu zao walikuwa wamewaandalia tayari. Zaidi ya hayo, wale waliokuwa karibu nao, hata mpaka kwa Isakari, na Zabuloni, na Naftali, wakaleta chakula juu ya punda, na ngamia, na nyumbu, na ng’ombe, vyakula vya unga, mikate ya tini, na vichala vya zabibu kavu, na divai, na mafuta, na ng’ombe, na kondoo tele; kwa kuwa kulikuwa na furaha katika Israeli.

1 Mambo ya Nyakati 12:1-40 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hawa ndio watu waliomjia Daudi huko Siklagi, wakati alikuwa amefukuzwa mbele ya Sauli mwana wa Kishi (walikuwa miongoni mwa mashujaa waliomsaidia Daudi vitani, walikuwa na pinde na walikuwa na uwezo wa kupiga mishale au kutupa mawe kwa kombeo wakitumia mkono wa kushoto au wa kulia; hawa walikuwa ndugu zake Sauli kutoka kabila la Benyamini): Mkuu wao alikuwa Ahiezeri, na wa pili Yoashi, wote wana wa Shemaa Mgibeathi; pia Yezieli na Peleti wana wa Azmawethi; Beraka, Yehu Mwanathothi, na Ishmaya Mgibeoni, shujaa miongoni mwa wale Thelathini, ambaye alikuwa kiongozi wa wale Thelathini; Yeremia, Yahazieli, Yohanani, Yozabadi, Mgederathi, Eluzai, Yeremothi, Bealia, Shemaria, Shefatia, Mharufi; Elikana, Ishia, Azareli, Yoezeri na Yashobeamu, wana wa Kora; Yoela na Zebadia, wana wa Yerohamu, kutoka Gedori. Baadhi ya Wagadi wakajitenga na kujiunga na Daudi katika ngome yake huko jangwani. Walikuwa mashujaa hodari, waliokuwa tayari kwa vita na wenye uwezo wa kutumia ngao na mkuki. Nyuso zao zilikuwa nyuso za simba na walikuwa na wepesi kama paa milimani. Ezeri alikuwa mkuu wao, Obadia alikuwa wa pili katika uongozi, Eliabu wa tatu, Mishmana wa nne, Yeremia wa tano, Atai wa sita, Elieli wa saba, Yohanani wa nane, Elzabadi wa tisa, Yeremia wa kumi, na Makbanai wa kumi na moja. Hawa Wagadi walikuwa majemadari. Aliyekuwa wa mwisho kuliko wote aliweza kuongoza askari 100, na aliyekuwa na uweza zaidi ya wote aliongoza 1,000. Wao ndio walivuka Mto Yordani katika mwezi wa kwanza ukiwa umefurika hadi kwenye kingo zake zote na kusababisha watu wote waliokuwa wanaishi kwenye mabonde kukimbilia mashariki na wengine magharibi. Wabenyamini wengine na baadhi ya watu kutoka Yuda pia walikuja kwa Daudi katika ngome yake. Daudi akatoka nje kuwalaki na akawaambia, “Kama mmekuja kwangu kwa amani, kunisaidia, mimi niko tayari kuwaruhusu ninyi kuungana nami. Lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa adui zangu wakati mimi mikono yangu haina hatia, basi Mungu wa baba zetu aone na awahukumu.” Kisha Roho akaja juu ya Amasai, mkuu wa wale Thelathini, naye akasema: “Sisi tu watu wako, ee Daudi! Nasi tuko pamoja na wewe, ee mwana wa Yese! Ushindi, naam, ushindi uwe kwako, pia ushindi kwa wale walio upande wako, kwa kuwa Mungu wako atakusaidia.” Kwa hiyo Daudi akawapokea na kuwafanya viongozi wa vikosi vyake vya uvamizi. Baadhi ya watu kutoka kabila la Manase wakajiunga na Daudi wakati alikwenda pamoja na Wafilisti, kupigana na Sauli. (Daudi na watu wake hawakuwasaidia Wafilisti kwa sababu, baada ya ushauri, watawala wao walimrudisha. Wakasema, “Itatugharimu vichwa vyetu kama Daudi atatuasi na kurudi kwa Sauli bwana wake.”) Daudi alipokwenda Siklagi, hawa ndio watu wa kabila la Manase waliojiunga naye: Adna, Yozabadi, Yediaeli, Mikaeli, Yozabadi, Elihu na Silethai, viongozi wa vikosi vya watu 1,000 katika kabila la Manase. Walimsaidia Daudi dhidi ya makundi ya uvamizi, kwa kuwa wote walikuwa mashujaa hodari na walikuwa majemadari katika jeshi lake. Siku baada ya siku watu walikuja kumsaidia Daudi, mpaka akawa na jeshi kubwa, kama jeshi la Mungu. Hawa ndio watu waliojiandaa kwa ajili ya vita waliokuja kwa Daudi huko Hebroni ili kumtwalia ufalme kutoka kwa Sauli, kama BWANA alivyokuwa amesema: watu wa Yuda, wanaochukua ngao na mikuki walikuwa 6,800 wote wakiwa tayari kwa vita. Watu wa Simeoni, mashujaa waliokuwa tayari kwa vita walikuwa 7,100. Watu wa Lawi walikuwa 4,600, pamoja na Yehoyada, kiongozi wa jamaa ya Aroni, aliyekuwa pamoja na watu 3,700, na Sadoki, kijana shujaa na hodari, aliyekuwa pamoja na maafisa ishirini na wawili kutoka jamaa yake. Watu wa Benyamini, ndugu zake Sauli, walikuwa 3,000; wengi wao walikuwa wameendelea kuwa waaminifu kwa Sauli mpaka wakati huo. Watu wa Efraimu, mashujaa hodari 20,800, watu waliokuwa maarufu katika koo zao. Watu wa nusu ya kabila la Manase, waliotajwa kwa majina ili waje kumweka Daudi kuwa mfalme, watu 18,000. Watu wa Isakari, waliofahamu majira na kujua kile ambacho Israeli inapasa kufanya, walikuwa viongozi 200, pamoja na jamaa zao wote chini ya uongozi wao. Watu wa Zabuloni, askari wenye uzoefu mkubwa walioandaliwa tayari kwa vita wakiwa na silaha za kila aina, ili kumsaidia Daudi kwa uaminifu thabiti, walikuwa 50,000. Watu wa Naftali, maafisa 1,000, pamoja na watu 37,000 waliochukua ngao na mikuki. Watu wa Dani 28,600 waliokuwa tayari kwa vita. Watu wa Asheri, askari 40,000 wenye uzoefu mkubwa waliondaliwa kwa ajili ya vita. Na pia watu kutoka mashariki ya Yordani, watu wa Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase, wakiwa na kila aina ya silaha, watu 120,000. Wote hawa walikuwa watu wapiganaji waliojitolea kutumika katika safu zao. Walikuja Hebroni wakiwa wameamua kikamilifu kumfanya Daudi mfalme juu ya Israeli yote. Waisraeli wengine wote walikuwa pia na nia hiyo moja ya kumfanya Daudi kuwa mfalme. Watu hawa wakakaa huko na Daudi siku tatu, wakila na kunywa, kwa sababu jamaa zao zilikuwa zimewapatia mahitaji yao. Pia, majirani zao hata wale walio mbali hadi Isakari, Zabuloni na Naftali, walikuja wakiwaletea vyakula walivyovibeba kwa punda, ngamia, nyumbu na maksai. Kulikuwepo na wingi wa unga, maandazi ya tini, maandazi ya zabibu kavu, divai, mafuta, ngʼombe na kondoo, kwa maana kulikuwa na furaha katika Israeli.