Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zek 1:7-17

Zek 1:7-17 SUV

Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani, mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema, Naliona wakati wa usiku, na tazama, mtu amepanda farasi mwekundu, akasimama kati ya mihadasi iliyokuwa mahali penye uvuli; na nyuma yake walikuwapo farasi wengine wekundu, na wa rangi ya kijivujivu, na weupe. Ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, ni nini hawa? Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Nitakuonyesha ni nini hawa. Na yule mtu aliyesimama kati ya mihadasi akajibu, akasema, Hawa ndio BWANA aliowatuma, waende huko na huko duniani. Nao wakamjibu yule malaika wa BWANA aliyesimama kati ya mihadasi, wakasema, Tumekwenda huko na huko duniani, na tazama, dunia yote inatulia, nayo imestarehe. Ndipo yule malaika wa BWANA akajibu, akasema, Ee BWANA wa majeshi, hata lini utakataa kuurehemu Yerusalemu, na miji ya Yuda uliyoikasirikia miaka hii sabini? Naye BWANA akamjibu yule malaika aliyesema nami kwa maneno mazuri, maneno yenye faraja. Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Haya, piga kelele na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Naona wivu kwa ajili ya Yerusalemu, na kwa ajili ya Sayuni; naona wivu mkuu sana. Nami ninawakasirikia sana mataifa wanaokaa hali ya raha; kwa maana mimi sikukasirika ila kidogo tu, na wao waliyahimiza mateso. Kwa sababu hiyo BWANA asema hivi, Ninaurudia Yerusalemu kwa rehema nyingi; nyumba yangu itajengwa ndani yake, asema BWANA wa majeshi, na kamba itanyoshwa juu ya Yerusalemu. Piga kelele tena, na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Miji yangu kwa kufanikiwa itaenezwa huko na huko tena; naye BWANA ataufariji Sayuni tena, atauchagua Yerusalemu tena.