Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 1:7-17

Zekaria 1:7-17 NENO

Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia mwana wa Ido. Wakati wa usiku nilipata maono, na tazama, mbele yangu palikuwa na mtu akiendesha farasi mwekundu! Alikuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi kwenye bonde. Nyuma yake walikuwepo farasi wekundu, wa kikahawia, na weupe. Nikauliza, “Hivi ni vitu gani bwana wangu?” Malaika aliyekuwa akizungumza na mimi akanijibu, “Nitakuonesha kuwa ni nini.” Kisha yule mtu aliyesimama katikati ya miti ya mihadasi akaeleza, “Ni wale ambao Mwenyezi Mungu amewatuma waende duniani kote.” Nao wakatoa taarifa kwa yule malaika wa Mwenyezi Mungu, aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumepita duniani kote na kukuta ulimwengu wote umepumzika kwa amani.” Kisha malaika wa Mwenyezi Mungu akasema, “Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, utazuia hadi lini rehema kutoka Yerusalemu na miji ya Yuda, ambayo umeikasirikia kwa miaka hii sabini?” Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akazungumza maneno ya upole na ya kufariji kwa malaika aliyezungumza nami. Kisha malaika yule aliyekuwa akizungumza nami akasema, “Tangaza neno hili: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Nina wivu sana kwa ajili ya Yerusalemu na Sayuni, lakini nimeyakasirikia sana mataifa yanayojisikia kuwa yako salama. Nilikuwa nimewakasirikia Israeli kidogo tu, lakini mataifa hayo yaliwazidishia maafa.’ “Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Nitairudia Yerusalemu kwa rehema na huko nyumba yangu itajengwa tena. Nayo kamba ya kupimia itanyooshwa juu ya Yerusalemu,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Endelea kutangaza zaidi kwamba: Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Miji yangu itafurika tena ustawi na Mwenyezi Mungu atamfariji tena Sayuni na kumchagua Yerusalemu.’ ”