Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 1:7-17

Zekaria 1:7-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi wa Shebati, mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia mimi nabii Zekaria mwana wa Berekia, mjukuu wa Ido, kama ifuatavyo: Wakati wa usiku, nilimwona malaika amepanda farasi mwekundu. Malaika huyo alikuwa amesimama bondeni, katikati ya miti ya mihadasi. Nyuma yake kulikuwa na farasi wengine wekundu, wa kijivujivu na weupe. Basi, nikamwuliza, “Bwana, Farasi hawa wanamaanisha nini?” Malaika huyo aliyeongea nami akaniambia, “Nitakuonesha hao farasi wanamaanisha nini. Hawa ndio waliotumwa na Mwenyezi-Mungu kuikagua dunia.” Hao farasi wakamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumeikagua dunia yote, nayo kweli imetulia.” Ndipo huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kwa muda gani utaendelea kutokuwa na huruma juu ya mji wa Yerusalemu na miji ya nchi ya Yuda ambayo umeikasirikia kwa muda wa miaka sabini?” Mwenyezi-Mungu akampa huyo malaika jibu jema na lenye matumaini. Basi, huyo malaika akaniambia, “Unapaswa kutangaza kwa sauti kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Moyo wangu umejaa upendo kwa mji wa Yerusalemu, naam, kwa mlima Siyoni. Walakini nimechukizwa sana na mataifa ambayo yanastarehe. Kweli niliwakasirikia Waisraeli kidogo, lakini mataifa hayo yaliwaongezea maafa. Kwa hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, naurudia mji wa Yerusalemu kwa huruma; humo itajengwa nyumba yangu, na ujenzi mpya wa mji utaanza.’” Kisha malaika huyo akaniambia nitangaze ujumbe huu mwingine: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Miji yangu itafurika tena fanaka. Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji tena mji wa Siyoni; nitauteua mji wa Yerusalemu kuwa wangu.’”

Shirikisha
Soma Zekaria 1

Zekaria 1:7-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani, mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema, Niliona wakati wa usiku, na tazama, mtu amepanda farasi mwekundu, akasimama kati ya miti ya mihadasi iliyokuwa mahali penye uvuli; na nyuma yake walikuwapo farasi wengine wekundu, na wa rangi ya kijivujivu, na weupe. Ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, ni nini hawa? Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Nitakuonesha ni nini hawa. Na yule mtu aliyesimama kati ya mihadasi akajibu, akasema, Hawa ndio BWANA aliowatuma, waende huku na huko duniani. Nao wakamjibu yule malaika wa BWANA aliyesimama kati ya mihadasi, wakasema, Tumekwenda huku na huko duniani, na tazama, dunia yote inatulia, nayo imestarehe. Ndipo yule malaika wa BWANA akajibu, akasema, Ee BWANA wa majeshi, hadi lini utakataa kuurehemu Yerusalemu, na miji ya Yuda uliyoikasirikia miaka hii sabini? Naye BWANA akamjibu yule malaika aliyesema nami kwa maneno mazuri, maneno yenye faraja. Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Haya, piga kelele na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Naona wivu kwa ajili ya Yerusalemu, na kwa ajili ya Sayuni; naona wivu mkuu sana. Nami ninayakasirikia sana mataifa yanayostarehe; kwa maana mimi nilikuwa nimekasirika kidogo tu, nao wakayazidisha maafa. Kwa sababu hiyo BWANA asema hivi, Ninaurudia Yerusalemu kwa rehema nyingi; nyumba yangu itajengwa ndani yake, asema BWANA wa majeshi, na kamba itanyoshwa juu ya Yerusalemu. Piga kelele tena, na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Miji yangu itajawa na ufanisi tena; naye BWANA ataufariji Sayuni tena, atauchagua Yerusalemu tena.

Shirikisha
Soma Zekaria 1

Zekaria 1:7-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani, mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema, Naliona wakati wa usiku, na tazama, mtu amepanda farasi mwekundu, akasimama kati ya mihadasi iliyokuwa mahali penye uvuli; na nyuma yake walikuwapo farasi wengine wekundu, na wa rangi ya kijivujivu, na weupe. Ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, ni nini hawa? Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Nitakuonyesha ni nini hawa. Na yule mtu aliyesimama kati ya mihadasi akajibu, akasema, Hawa ndio BWANA aliowatuma, waende huko na huko duniani. Nao wakamjibu yule malaika wa BWANA aliyesimama kati ya mihadasi, wakasema, Tumekwenda huko na huko duniani, na tazama, dunia yote inatulia, nayo imestarehe. Ndipo yule malaika wa BWANA akajibu, akasema, Ee BWANA wa majeshi, hata lini utakataa kuurehemu Yerusalemu, na miji ya Yuda uliyoikasirikia miaka hii sabini? Naye BWANA akamjibu yule malaika aliyesema nami kwa maneno mazuri, maneno yenye faraja. Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Haya, piga kelele na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Naona wivu kwa ajili ya Yerusalemu, na kwa ajili ya Sayuni; naona wivu mkuu sana. Nami ninawakasirikia sana mataifa wanaokaa hali ya raha; kwa maana mimi sikukasirika ila kidogo tu, na wao waliyahimiza mateso. Kwa sababu hiyo BWANA asema hivi, Ninaurudia Yerusalemu kwa rehema nyingi; nyumba yangu itajengwa ndani yake, asema BWANA wa majeshi, na kamba itanyoshwa juu ya Yerusalemu. Piga kelele tena, na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Miji yangu kwa kufanikiwa itaenezwa huko na huko tena; naye BWANA ataufariji Sayuni tena, atauchagua Yerusalemu tena.

Shirikisha
Soma Zekaria 1

Zekaria 1:7-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario, neno la BWANA lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia mwana wa Ido. Wakati wa usiku nilipata maono, mbele yangu alikuwepo mtu akiendesha farasi mwekundu! Alikuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi kwenye bonde. Nyuma yake walikuwepo farasi wekundu, wa kikahawia na weupe. Nikauliza, “Hivi ni vitu gani bwana wangu?” Malaika aliyekuwa akizungumza na mimi akanijibu, “Nitakuonyesha kuwa ni nini.” Kisha yule mtu aliyesimama katikati ya miti ya mihadasi akaeleza, “Ni wale ambao BWANA amewatuma waende duniani kote.” Nao wakatoa taarifa kwa yule malaika wa BWANA, aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumepita duniani kote na kukuta ulimwengu wote umepumzika kwa amani.” Kisha malaika wa BWANA akasema, “BWANA Mwenye Nguvu Zote, utazuia mpaka lini rehema kutoka Yerusalemu na miji ya Yuda, ambayo umeikasirikia kwa miaka hii sabini?” Kwa hiyo BWANA akazungumza maneno ya upole na ya kufariji kwa malaika aliyezungumza nami. Kisha malaika yule aliyekuwa akizungumza nami akasema, “Tangaza neno hili: Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote asemalo: ‘Nina wivu sana kwa ajili ya Yerusalemu na Sayuni, lakini nimeyakasirikia sana mataifa yanayojisikia kuwa yako salama. Nilikuwa nimewakasirikia Israeli kidogo tu, lakini mataifa hayo yaliwazidishia maafa.’ “Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo BWANA: ‘Nitairudia Yerusalemu kwa rehema na huko nyumba yangu itajengwa tena. Nayo kamba ya kupimia itanyooshwa Yerusalemu,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. “Endelea kutangaza zaidi kwamba: Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: ‘Miji yangu itafurika tena ustawi na BWANA atamfariji tena Sayuni na kumchagua Yerusalemu.’ ”

Shirikisha
Soma Zekaria 1