Mit 21:1-13
Mit 21:1-13 SUV
Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa BWANA; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo. Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali BWANA huipima mioyo. Kutenda haki na hukumu Humpendeza BWANA kuliko kutoa sadaka. Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, Hata ukulima wa waovu, ni dhambi. Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji. Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti. Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu. Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana; Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa. Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi. Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili machoni pake. Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa. Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia. Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa.