Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 21:1-13

Mithali 21:1-13 NENO

Moyo wa mfalme uko katika mkono wa Mwenyezi Mungu; huuongoza kama mkondo wa maji, popote apendapo. Njia zote za mwanadamu huonekana sawa kwake, bali Mwenyezi Mungu huupima moyo. Kufanya yaliyo sawa na haki inakubalika zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko dhabihu. Macho ya kudharau na moyo wa kiburi, ambavyo ni taa ya waovu, vyote ni dhambi! Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida, kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini. Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha. Jeuri ya waovu itawaburuta mbali, kwa kuwa wanakataa kufanya yaliyo sawa. Njia ya mwenye hatia ni ya upotovu, bali tabia ya mtu asiye na hatia ni nyofu. Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi. Mtu mwovu hutamani sana ubaya, jirani yake hapati huruma kutoka kwake. Wakati mwenye mzaha ameadhibiwa, mjinga hupata hekima; wakati mtu mwenye hekima anafundishwa, hupata maarifa. Mwenye Haki huyajua yanayotendeka katika nyumba za waovu, naye atawaangamiza waovu. Mtu akiziba masikio asisikie kilio cha maskini, yeye pia atalia, wala hatajibiwa.