Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 21

21
1Moyo wa mfalme uko katika mkono wa Mwenyezi Mungu;
huuongoza kama mkondo wa maji, popote apendapo.
2Njia zote za mwanadamu huonekana sawa kwake,
bali Mwenyezi Mungu huupima moyo.
3Kufanya yaliyo sawa na haki inakubalika
zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko dhabihu.
4Macho ya kudharau na moyo wa kiburi,
ambavyo ni taa ya waovu, vyote ni dhambi!
5Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida,
kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini.
6Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo
ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha.
7Jeuri ya waovu itawaburuta mbali,
kwa kuwa wanakataa kufanya yaliyo sawa.
8Njia ya mwenye hatia ni ya upotovu,
bali tabia ya mtu asiye na hatia ni nyofu.
9Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba,
kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.
10Mtu mwovu hutamani sana ubaya,
jirani yake hapati huruma kutoka kwake.
11Wakati mwenye mzaha ameadhibiwa,
mjinga hupata hekima;
wakati mtu mwenye hekima anafundishwa,
hupata maarifa.
12Mwenye Haki huyajua yanayotendeka katika nyumba za waovu,
naye atawaangamiza waovu.
13Mtu akiziba masikio asisikie kilio cha maskini,
yeye pia atalia, wala hatajibiwa.
14Zawadi inayotolewa kwa siri hutuliza hasira,
na rushwa iliyofichwa kwenye nguo hutuliza ghadhabu kali.
15Wakati haki imetendeka, huleta furaha kwa wenye haki,
bali hofu kwa watenda maovu.
16Mtu anayepotea kutoka mapito ya ufahamu,
hupumzika katika kundi la waliokufa.
17Mtu apendaye anasa atakuwa maskini,
yeyote apendaye mvinyo na mafuta kamwe hatakuwa tajiri.
18Waovu huwa fidia kwa ajili ya wenye haki,
nao wasio waaminifu kwa ajili ya wanyofu.
19Ni afadhali kuishi jangwani
kuliko kuishi na mke mgomvi na mkorofi.
20Katika nyumba ya mwenye hekima
kuna akiba ya vyakula vizuri na mafuta,
lakini mtu mpumbavu
hutafuna vyote alivyo navyo.
21Yeye afuatiaye haki na upendo
hupata uzima, mafanikio na heshima.
22Mtu mwenye hekima huushambulia mji wa wenye nguvu,
na kuangusha ngome wanazozitegemea.
23Yeye alindaye kinywa chake na ulimi wake
hujilinda na maafa.
24Mtu mwenye kiburi na majivuno, “Mdhihaki” ndilo jina lake;
hutenda mambo kwa kiburi kilichozidi.
25Kutamani sana kwa mvivu kutakuwa kifo chake,
kwa sababu mikono yake haitaki kufanya kazi.
26Mchana kutwa hutamani zaidi,
lakini mnyofu hutoa pasipo kuzuia.
27Dhabihu ya mtu mwovu ni chukizo;
si ni chukizo zaidi ikitolewa kwa nia mbaya!
28Shahidi wa uongo ataangamia,
bali maneno ya mwenye kusikia yatadumu.
29Mtu mwovu ana uso wa ushupavu,
bali mtu mnyofu huzifikiria njia zake.
30Hakuna hekima, wala akili, wala mpango
unaoweza kufaulu dhidi ya Mwenyezi Mungu.
31Farasi huandaliwa kwa ajili ya siku ya vita,
bali ushindi huwa kwa Mwenyezi Mungu.

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 21: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia