Hes 13:21-33
Hes 13:21-33 SUV
Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hata Rehobu, mpaka kuingia Hamathi. Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri. Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini. Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli. Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini. Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi. Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani. Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.