Hesabu 13:21-33
Hesabu 13:21-33 NEN
Hivyo wakapanda na kuipeleleza nchi kutoka Jangwa la Sini hadi Rehobu, kuelekea Lebo-Hamathi. Wakapanda kupitia Negebu hadi wakafika Hebroni, mahali ambapo Ahimani, Sheshai na Talmai, wazao wa Anaki, waliishi. (Hebroni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya mji wa Soani ulioko Misri.) Walipofika katika Bonde la Eshkoli, walivunja tawi lililokuwa na kishada kimoja cha zabibu. Wawili wao wakalichukua lile tawi kwenye mti, pamoja na komamanga na tini. Eneo lile likaitwa Bonde la Eshkoli kwa sababu ya kile kishada cha zabibu ambacho Waisraeli walikikata huko. Mwishoni mwa siku arobaini wakarudi kutoka kuipeleleza nchi. Wakarudi kwa Mose, Aroni na jumuiya yote ya Waisraeli huko Kadeshi kwenye Jangwa la Parani. Hapo ndipo walipotoa habari kwao na kwa kusanyiko lote na kuwaonyesha matunda ya hiyo nchi. Wakampa Mose taarifa hii: “Tuliingia katika nchi uliyotutuma, nayo inatiririka maziwa na asali! Hili hapa tunda lake. Lakini watu wanaoishi huko ni wenye nguvu, na miji yao ina ngome na ni mikubwa sana. Huko tuliona hata wazao wa Anaki. Waamaleki wanaishi Negebu; Wahiti, Wayebusi na Waamori wanaishi katika nchi ya vilima; nao Wakanaani wanaishi karibu na bahari na kando ya Yordani.” Kisha Kalebu akawanyamazisha watu mbele ya Mose na kusema, “Imetupasa kupanda na kuimiliki nchi, kwa maana hakika tunaweza kufanya hivyo.” Lakini watu waliokuwa wamepanda pamoja naye wakasema, “Hatuwezi kuwashambulia wale watu; wana nguvu kutuliko sisi.” Wakaeneza taarifa mbaya miongoni mwa Waisraeli kuhusu nchi waliyoipeleleza. Wakasema, “Nchi tuliyoipeleleza hula watu waishio ndani yake. Watu wote tuliowaona huko ni majitu. Tuliwaona Wanefili huko (wazao wa Anaki wanatokana na Wanefili.) Tulijiona kama panzi machoni petu wenyewe, nao ndivyo walivyotuona.”