Mk 7:14-37
Mk 7:14-37 SUV
Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. [ Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.] Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi. Akaondoka huko, akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika. Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake. Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake. Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa. Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto. Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako. Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka. Akatoka tena katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.