Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 7:14-37

Marko 7:14-37 NENO

Isa akaita tena umati ule wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, na mwelewe jambo hili. Hakuna kitu kinachomwingia mtu kimtiacho unajisi, lakini kile kimtokacho ndicho kimtiacho unajisi. [ Kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia na asikie.]” Baada ya Isa kuacha ule umati wa watu na kuingia ndani, wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano ule. Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi? Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Isa alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni safi.) Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.” Ndipo Isa akaondoka hapo akaenda sehemu za Tiro. Akaingia katika nyumba moja, naye hakutaka mtu yeyote ajue kwamba yuko humo. Lakini hakuweza kujificha. Mara mwanamke mmoja, ambaye binti yake mdogo alikuwa na pepo mchafu, akaja na kumpigia magoti miguuni pake. Basi huyo mwanamke alikuwa Myunani, aliyezaliwa Foinike ya Siria. Akamsihi Isa amtoe binti yake huyo pepo mchafu. Isa akamwambia, “Waache watoto washibe kwanza, kwa maana si vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Lakini yule mwanamke akamjibu, “Bwana, hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya chakula cha watoto.” Ndipo Isa akamjibu, “Kwa sababu ya jibu lako, nenda zako nyumbani; yule pepo mchafu amemtoka binti yako.” Akaenda zake nyumbani akamkuta binti yake amelala kitandani, yule pepo mchafu akiwa amemtoka. Kisha Isa akaondoka sehemu za Tiro, akapita katikati ya Sidoni, hadi Bahari ya Galilaya na kuingia eneo la Dekapoli. Huko, watu wakamletea Isa mtu mmoja kiziwi, ambaye pia alikuwa na kigugumizi, wakamwomba aweke mkono wake juu ya huyo mtu. Isa akampeleka yule kiziwi kando, mbali na watu, akatia vidole vyake masikioni mwa yule mtu. Kisha akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. Ndipo Isa akatazama mbinguni, akashusha pumzi kwa nguvu, akamwambia, “Efatha!” (yaani, “Funguka!”) Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukaachiliwa, akaanza kuongea sawasawa. Isa akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hizi. Lakini kadiri alivyowakanya, ndivyo walivyozidi kutangaza kwa bidii. Walistaajabu mno. Wakasema, “Amefanya mambo yote vizuri mno! Amewawezesha viziwi wasikie na bubu waseme!”

Video zinazohusiana