Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mk 14:26-42

Mk 14:26-42 SUV

Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni. Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile. Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo. Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe. Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja? Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu. Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo. Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu. Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia.