Mt 21:10-22
Mt 21:10-22 SUV
Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu? Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya. Yesu akaingia ndani ya hekalu, akawafukuza wote waliokuwa wakiuza na kununua hekaluni, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza njiwa; akawaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Na vipofu na viwete wakamwendea mle hekaluni, akawaponya. Lakini wakuu wa makuhani na waandishi walipoyaona maajabu aliyoyafanya, na watoto waliopaza sauti zao hekaluni, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi! Walikasirika, wakamwambia, Wasikia hawa wasemavyo? Yesu akawaambia, Naam; hamkupata kusoma, Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umekamilisha sifa? Akawaacha, akatoka nje ya mji mpaka Bethania, akalala huko. Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini, aliona njaa. Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia, Yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele. Mtini ukanyauka mara. Wanafunzi walipoona, walistaajabu, wakisema, Jinsi gani mtini umenyauka mara? Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng’oka, ukatupwe baharini, litatendeka. Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.