Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 21:10-22

Mathayo 21:10-22 NEN

Yesu alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, “Huyu ni nani?” Ule umati wa watu ukajibu, “Huyu ni Yesu, yule nabii kutoka Nazareti katika Galilaya.” Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyangʼanyi.” Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya. Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walipoona mambo ya ajabu aliyofanya na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika. Wakamuuliza Yesu, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?” Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma, “ ‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao umeamuru sifa’?” Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko. Asubuhi na mapema, Yesu alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa. Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka. Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?” Yesu akawajibu, “Amin, nawaambia, kama mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ngʼoka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”