Ayu 37:1-13
Ayu 37:1-13 SUV
Moyo wangu hunitetema kwayo pia, Nao hutoka mahali pake. Zisikizeni hizo kelele za sauti yake, Na uvumi utokao kinywani mwake. Yeye huituma iende chini ya mbingu zote, Na radi yake hata miisho ya nchi. Baadaye sauti hunguruma; Yeye hunguruma kwa sauti ya ukuu wake; Hazizuii hapo sauti yake isikiwapo. Mungu hunguruma kwa kustaajabisha kwa sauti yake; Hufanya mambo makuu, ambayo hatuwezi kuelewa nayo. Kwani huiambia theluji, Anguka juu ya nchi; Na vivyo manyonyota ya mvua, Na hayo maji ya mvua yake kubwa. Huufunga mkono wa kila binadamu; Ili watu wote aliowaumba wajue. Hapo wanyama huingia mafichoni, Na kukaa katika mapango yao. Dhoruba hutoka katika vyumba vyake; Na baridi ghalani mwake. Barafu huletwa kwa pumzi za Mungu; Na upana wa maji huganda. Naam, huyatweka mawingu mazito mzigo wa maji; Hulitandika wingu la umeme wake; Nalo hugeuzwa huku na huku kwa uongozi wake, Ili yafanye yote atakayoyaagiza Juu ya uso wa dunia hii ikaayo watu; Kama ni kwa kuonya, au kama ni kwa nchi yake, Au kama ni kwa rehema, ndiye aletaye.