Yobu 37:1-13
Yobu 37:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kutokana na hayo, moyo wangu unatetemeka, na kuruka kutoka mahali pake. Sikilizeni ngurumo ya sauti ya Mungu, na mvumo wa sauti kutoka kinywani mwake. Huufanya uenee chini ya mbingu yote, umeme wake huueneza pembe zote za dunia. Ndipo sauti yake hunguruma, sauti ya Mungu hunguruma kwa fahari na muda huo wote umeme humulikamulika. Mungu hupiga radi ya ajabu kwa sauti yake, hufanya mambo makuu tusiyoweza kuyaelewa. Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya nchi!’ Na manyunyu na mvua, ‘Nyesha kwa nguvu.’ Hufunga shughuli za kila mtu; ili watu wote watambue kazi yake. Wanyama wa porini hurudi mafichoni mwao, na hubaki katika mapango yao. Dhoruba huvuma kutoka chumba chake, na baridi kali kutoka ghalani mwake. Kwa pumzi ya Mungu barafu hutokea, uso wa maji huganda kwa haraka. Mungu hulijaza wingu manyunyu mazito; mawingu husambaza umeme wake. Kwa amri yake vyote huzunguka huku na huko, kutekeleza kila kitu anachokiamuru, kufanyika katika ulimwengu wa viumbe. Mungu hutekeleza matakwa yake duniani; iwe ni kwa ajili ya kuwaadhibu watu, au kwa ajili ya kuonesha upendo wake.
Yobu 37:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Moyo wangu hutetemeka kwa hayo pia, Nao huruka kutoka mahali pake. Zisikizeni hizo kelele za sauti yake, Na uvumi utokao kinywani mwake. Yeye huituma iende chini ya mbingu zote, Na radi yake hata miisho ya nchi. Baadaye sauti hunguruma; Yeye hunguruma kwa sauti ya ukuu wake; Hazizuii hapo sauti yake isikiwapo. Mungu hunguruma kwa kustaajabisha kwa sauti yake; Hufanya mambo makuu, ambayo hatuwezi kuyaelewa. Kwa kuwa huiambia theluji, Anguka juu ya nchi; Na pia kwa manyunyu ya mvua, Hayo manyunyu ya mvua yake nyingi. Huufunga mkono wa kila binadamu; Ili watu wote aliowaumba wajue. Hapo wanyama huingia mafichoni, Na kukaa katika mapango yao. Dhoruba hutoka katika vyumba vyake; Na baridi ghalani mwake. Kwa pumzi ya Mungu barafu hutokea; Na uso wa maji huganda punde. Naam, huyatwika mawingu mazito mzigo wa maji; Hulitandika wingu la umeme wake; Nalo hugeuzwa huku na huku kwa uongozi wake, Ili yafanye yote atakayoyaagiza Juu ya uso wa dunia hii ikaayo watu; Kama ni kwa kuonya, au kama ni kwa nchi yake, Au kama ni kwa rehema, ndiye aletaye.
Yobu 37:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Moyo wangu hunitetema kwayo pia, Nao hutoka mahali pake. Zisikizeni hizo kelele za sauti yake, Na uvumi utokao kinywani mwake. Yeye huituma iende chini ya mbingu zote, Na radi yake hata miisho ya nchi. Baadaye sauti hunguruma; Yeye hunguruma kwa sauti ya ukuu wake; Hazizuii hapo sauti yake isikiwapo. Mungu hunguruma kwa kustaajabisha kwa sauti yake; Hufanya mambo makuu, ambayo hatuwezi kuelewa nayo. Kwani huiambia theluji, Anguka juu ya nchi; Na vivyo manyonyota ya mvua, Na hayo maji ya mvua yake kubwa. Huufunga mkono wa kila binadamu; Ili watu wote aliowaumba wajue. Hapo wanyama huingia mafichoni, Na kukaa katika mapango yao. Dhoruba hutoka katika vyumba vyake; Na baridi ghalani mwake. Barafu huletwa kwa pumzi za Mungu; Na upana wa maji huganda. Naam, huyatweka mawingu mazito mzigo wa maji; Hulitandika wingu la umeme wake; Nalo hugeuzwa huku na huku kwa uongozi wake, Ili yafanye yote atakayoyaagiza Juu ya uso wa dunia hii ikaayo watu; Kama ni kwa kuonya, au kama ni kwa nchi yake, Au kama ni kwa rehema, ndiye aletaye.
Yobu 37:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Kwa hili moyo wangu unatetemeka, nao unaruka kutoka mahali pake. Sikiliza! Sikiliza ngurumo ya sauti yake, sauti ya ngurumo inayotoka kinywani mwake. Huuachilia umeme wake wa radi chini ya mbingu yote na kuupeleka hata miisho ya dunia. Baada ya hayo huja sauti ya ngurumo yake; Mungu hunguruma kwa sauti yake ya fahari. Wakati sauti yake inanguruma tena, huuachilia umeme wake wa radi. Sauti ya Mungu hunguruma kwa namna za ajabu; yeye hutenda mambo makuu kupita ufahamu wetu. Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya dunia,’ nayo manyunyu ya mvua, ‘Uwe mvua ya nguvu.’ Ili wanadamu wote aliowaumba wapate kujua kazi zake, yeye humzuilia kila mtu shughuli zake. Wanyama hujificha; hubakia kwenye mapango yao. Dhoruba hutoka katika chumba chake, baridi hutoka katika upepo uendao kasi. Pumzi ya Mungu hutoa barafu, eneo kubwa la maji huganda. Huyasheheneza mawingu kwa maji, naye husambaza umeme wake wa radi kupitia hayo. Nayo mawingu huzungukazunguka pande zote kwa amri yake, juu ya uso wa dunia yote, kufanya lolote ayaamuruyo. Huleta mawingu ili kuadhibu wanadamu, au kuinyeshea dunia yake na kuonesha upendo wake.