Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayu 28:1-19

Ayu 28:1-19 SUV

Hakika kuna shimo wachimbako fedha, Na mahali wapatapo dhahabu waisafishayo. Chuma hufukuliwa katika ardhi, Na shaba huyeyushwa katika mawe. Binadamu hukomesha giza; Huyatafuta-tafuta hata mpaka ulio mbali, Mawe ya giza kuu, giza tupu. Hufukua shimo mbali na makao ya watu; Husahauliwa na nyayo zipitazo; Huning’inia mbali na watu, huyumba-yumba huko na huko. Katika ardhi ndimo kitokeamo chakula; Na chini yake hupinduliwa kama kwa moto. Mawe yake ni mahali zipatikanapo yakuti; Nayo ina mchanga wa dhahabu. Njia ile hapana ndege mkali aijuaye, Wala jicho la tai halijaiona; Wanyama wakali wajivunao hawajaikanyaga, Wala simba mkali hajaipita. Huunyoshea mwamba wa gumegume mkono wake; Huipindua milima hata misingi yake. Hukata mifereji kati ya majabali; Na jicho lake huona kila kito cha thamani Hufunga vijito visichuruzike; Na kitu kilichostirika hukifunua. Bali hekima itapatikana wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi? Mwanadamu hajui thamani yake, Wala haionekani katika nchi ya walio hai. Vilindi vyasema, Haimo ndani yangu; Na bahari yasema, Haiko kwangu. Haipatikani kwa dhahabu, Wala fedha haitapimwa iwe thamani yake. Haiwezi kutiwa thamani kwa dhahabu ya Ofiri, Wala kwa shohamu ya thamani nyingi, wala kwa yakuti ya samawi. Dhahabu na vioo haviwezi kulinganishwa nayo; Wala kubadili kwake hakutakuwa kwa vyombo vya dhahabu safi. Havitatajwa fedhaluka wala bilauri; Naam, kima cha hekima chapita marijani. Yakuti ya rangi ya manjano ya Kushi haitasawazishwa nayo, Wala haitatiwa kima kwa dhahabu safi.