Ayu 24:13-25
Ayu 24:13-25 SUV
Hawa ni katika hao waliouasi mwanga; Hawazijui njia zake, Wala hawakai katika mapito yake. Mwuaji huamka asubuhi kukipambauka, huwaua maskini na wahitaji; Tena wakati wa usiku yu kama mwivi. Tena jicho lake mzinifu hungojea wakati wa giza-giza, Akisema, Hapana jicho litakaloniona; Naye huuficha uso wake. Wao hutoboa nyumba gizani; Hujifungia ndani wakati wa mchana; Hawaujui mwanga. Kwani asubuhi kwao wote ni kama giza tupu; Kwani wao wavijua vitisho vya hiyo giza tupu. Mwasema, Yeye ni mwepesi juu ya uso wa gharika; Sehemu yao inalaaniwa duniani; Hageuki kwenda njia ya mizabibuni. Chaka na hari hukausha maji ya theluji; Kuzimu nako hao ambao wamefanya dhambi. Tumbo lililomzaa litamsahau; buu litamla na kuona tamu; Hatakumbukwa tena; Na udhalimu utavunjwa kama mti. Naam, yeye huwala walio tasa wasiozaa; Wala hamtendei mema mwanamke mjane. Lakini Mungu huwadumisha wenye uwezo kwa nguvu zake; Huinuka, wasiokuwa na tumaini la kuishi. Huwapa kuwa na salama, nao wapumzika kwayo; Na macho yake ya juu ya njia zao. Wao wametukuzwa; lakini kitambo kidogo hutoweka; Naam, hushushwa, na kuondolewa njiani kama wengine wote, Nao hukatwa kama vile masuke ya ngano. Na kama sivyo sasa, ni nani atakayenihukumu kuwa ni mwongo, Na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?