Yobu 24:13-25
Yobu 24:13-25 Biblia Habari Njema (BHN)
“Wapo wengine waovu wasiopenda mwanga, wasiozifahamu njia za mwanga, na hawapendi kuzishika njia zake. Mwuaji huamka mapema alfajiri, ili kwenda kuwaua maskini na fukara, na usiku ukifika, kazi yake ni kuiba. Mzinifu naye hungojea giza liingie; akisema, ‘Hakuna atakayeniona;’ kisha huuficha uso wake kwa nguo. Usiku wezi huvunja nyumba, lakini mchana hujifungia ndani; wala hawajui kabisa mwanga ni nini. Kwao wote giza nene ni mwanga wa asubuhi; wao ni marafiki wa vitisho vya giza nene. “Lakini mwasema: ‘Waovu huchukuliwa haraka na mafuriko ya maji, makao yao hubaki kuwa nchi iliyolaaniwa; hakuna aendaye kwenye mashamba yao ya mizabibu.’ Kama theluji inavyoyeyuka katika joto na ukame ndivyo Kuzimu kunavyowanyakua waovu. Maana mzazi wao huwasahau watu hao, hakuna atakayewakumbuka tena. Ndivyo uovu ulivyovunjwa kama mti. “Waovu huwadhulumu wanawake wasiopata watoto. Wala hawawatendei wema wanawake wajane. Mungu, kwa nguvu yake huwaangamiza wenye uwezo, huinuka nao hukata tamaa ya kuishi. Huwaacha waovu wajione salama, lakini macho yake huchunguza mienendo yao. Waovu hufana kwa muda tu, kisha hutoweka, hunyauka na kufifia kama jani, hukatiliwa mbali kama masuke ya ngano. Nani basi, awezaye kuhakikisha kuwa mimi ni mwongo na kuonesha kwamba maneno yangu si kweli?”
Yobu 24:13-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hawa ni katika hao waliouasi mwanga; Hawazijui njia zake, Wala hawakai katika mapito yake. Mwuaji huamka asubuhi kukipambazuka, huwaua maskini na wahitaji; Tena wakati wa usiku yu kama mwizi. Tena jicho lake mzinifu hungojea wakati wa gizagiza, Akisema, Hapana jicho litakaloniona; Naye huuficha uso wake. Wao hutoboa nyumba gizani; Hujifungia ndani wakati wa mchana; Hawaujui mwanga. Maana asubuhi kwao wote ni kama giza tupu; Maana wao wavijua vitisho vya hiyo giza tupu. Mwasema, Yeye ni mwepesi juu ya uso wa gharika; Sehemu yao inalaaniwa duniani; Hageuki kwenda njia ya mizabibuni. Ukame na joto hukausha maji ya theluji; Kama kuzimu kuwafanyavyo watenda dhambi. Tumbo lililomzaa litamsahau; buu litamla na kuona tamu; Hatakumbukwa tena; Na udhalimu utavunjwa kama mti. Naam, yeye huwala walio tasa wasiozaa; Wala hamtendei mema mwanamke mjane. Lakini Mungu huwadumisha wenye uwezo kwa nguvu zake; Huinuka, wasiokuwa na tumaini la kuishi. Huwapa usalama, nao wapumzika kwao; Na macho yake yako juu ya njia zao. Wao wametukuzwa; lakini kitambo kidogo hutoweka; Naam, hushushwa, na kuondolewa njiani kama wengine wote, Nao hukatwa kama vile masuke ya ngano. Na kama sivyo sasa, ni nani atakayenihukumu mimi kuwa ni mwongo, Na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?
Yobu 24:13-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hawa ni katika hao waliouasi mwanga; Hawazijui njia zake, Wala hawakai katika mapito yake. Mwuaji huamka asubuhi kukipambauka, huwaua maskini na wahitaji; Tena wakati wa usiku yu kama mwivi. Tena jicho lake mzinifu hungojea wakati wa giza-giza, Akisema, Hapana jicho litakaloniona; Naye huuficha uso wake. Wao hutoboa nyumba gizani; Hujifungia ndani wakati wa mchana; Hawaujui mwanga. Kwani asubuhi kwao wote ni kama giza tupu; Kwani wao wavijua vitisho vya hiyo giza tupu. Mwasema, Yeye ni mwepesi juu ya uso wa gharika; Sehemu yao inalaaniwa duniani; Hageuki kwenda njia ya mizabibuni. Chaka na hari hukausha maji ya theluji; Kuzimu nako hao ambao wamefanya dhambi. Tumbo lililomzaa litamsahau; buu litamla na kuona tamu; Hatakumbukwa tena; Na udhalimu utavunjwa kama mti. Naam, yeye huwala walio tasa wasiozaa; Wala hamtendei mema mwanamke mjane. Lakini Mungu huwadumisha wenye uwezo kwa nguvu zake; Huinuka, wasiokuwa na tumaini la kuishi. Huwapa kuwa na salama, nao wapumzika kwayo; Na macho yake ya juu ya njia zao. Wao wametukuzwa; lakini kitambo kidogo hutoweka; Naam, hushushwa, na kuondolewa njiani kama wengine wote, Nao hukatwa kama vile masuke ya ngano. Na kama sivyo sasa, ni nani atakayenihukumu kuwa ni mwongo, Na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?
Yobu 24:13-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Wako wale wanaoiasi nuru, wasiofahamu njia zake wala hawakai katika mapito yake. Wakati mwanga wa mchana unapotoweka, muuaji huinuka naye huwaua maskini na mhitaji; wakati wa usiku hunyemelea kama mwizi. Jicho la mzinzi hungojea wakati wa giza, naye hufikiri, ‘Hakuna jicho litakaloniona,’ naye huuficha uso wake. Katika giza, huvunja majumba, lakini wakati wa mchana hujifungia ndani; hawataki kufanya lolote nuruni. Kwa wote hawa, giza nene ndiyo asubuhi yao; hujifanya rafiki na vitisho vya gizani. “Lakini wao ni povu juu ya maji; sehemu yao juu ya nchi imelaaniwa, hivyo hakuna hata mmoja aendaye kwenye shamba la mizabibu. Kama vile joto na hari vinyakuavyo theluji iliyoyeyuka, ndivyo kuzimu kuwanyakuavyo waliotenda dhambi. Tumbo lililowazaa huwasahau, nao huwa karamu ya mabuu; watu waovu hawakumbukwi tena, lakini huvunjika kama mti. Huwafanya mawindo wanawake tasa na wasio na watoto, nao hawaonyeshi huruma kwa wajane. Lakini Mungu huwakokota wenye nguvu kwa uwezo wake; ingawa wamestawi, hawana hakika ya maisha. Aweza akawaacha wakapumzika wakijihisi salama, lakini macho yake yanaona njia zao. Kwa kitambo kidogo hutukuka, hatimaye hutoweka; hushushwa na kukusanywa kama wengine wote, hukatwa kama masuke ya nafaka. “Kama hili sivyo, ni nani awezaye kunithibitisha kuwa mwongo, na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?”