Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isa 30:8-26

Isa 30:8-26 SUV

Haya, enenda sasa, andika neno hili katika kibao mbele ya macho yao, lichore katika kitabu ili liwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele. Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA; wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo; tokeni katika njia, geukeni mtoke katika mapito; mkomesheni Mtakatifu wa Israeli mbele yetu. Basi kwa ajili ya hayo Mtakatifu wa Israeli asema hivi, Kwa sababu mwalidharau neno hili, na kutumainia jeuri na ukaidi, na kuyategemea hayo; basi, uovu huu utakuwa kwenu kama mahali palipobomoka, palipo tayari kuanguka patokezapo katika ukuta mrefu, ambapo kuvunjika kwake huja ghafula kwa mara moja. Naye atapavunja kama chombo cha mfinyanzi kivunjwavyo, akikivunja-vunja asiache kukivunja, hata hakipatikani katika vipande vyake kigae kitoshacho kutwaa moto jikoni, au kuteka maji kisimani. Kwa maana Bwana MUNGU, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi, Kwa kurudi na kustarehe mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini; lakini hamkukubali. Bali ninyi mlisema, La! Maana tutakimbia juu ya farasi; basi, ni kweli, mtakimbia; tena, Sisi tutakimbia juu ya wanyama waendao upesi; basi, wale watakaowafuatia watakuwa wepesi. Elfu moja watakimbia kwa kukemewa na mtu mmoja; kwa kukemewa na watano mtakimbia; hata mtakapoachwa kama mlingoti juu ya kilele cha mlima, na kama bendera juu ya kilima. Kwa ajili ya hayo BWANA atangoja, ili awaonee huruma, na kwa ajili ya hayo atatukuzwa, ili awarehemu; kwa maana BWANA ni Mungu wa hukumu; heri wote wamngojao. Kwa maana watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu. Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto. Nanyi mtakitia najisi kifuniko cha sanamu zenu za fedha zilizochongwa, na mabamba ya sanamu zenu za dhahabu zilizoyeyushwa; utazitupilia mbali kama kitu kilicho najisi; utasema, Haya, toka hapa. Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng’ombe zako watakula katika malisho mapana. Ng’ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo. Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara. Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile BWANA atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.

Soma Isa 30