Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 30:8-26

Isaya 30:8-26 Biblia Habari Njema (BHN)

Mungu aliniambia: “Sasa chukua kibao cha kuandikia, uandike jambo hili mbele yao, liwe ushahidi wa milele: Watu hawa ni waasi, watoto wasioaminika; watu wasiopenda kusikia mafunzo ya Mwenyezi-Mungu. Huwaambia waonaji: ‘Msione maono’, na manabii: ‘Msitutangazie ukweli, bali tuambieni mambo ya kupendeza, toeni unabii wa mambo ya udanganyifu tu. Geukeni na kuiacha njia ya ukweli; msituambie tena juu ya Mungu, Mtakatifu wa Israeli.’” Kwa hiyo Mungu, Mtakatifu wa Israeli asema: “Nyinyi mmeukataa ujumbe wangu; mkapania kufanya dhuluma na udanganyifu. Basi, dhambi hii itawaleteeni maangamizi kama ufa mkubwa katika ukuta mrefu; utabomoka mara na kuanguka chini ghafla. Kuporomoka kwa ukuta huo, ni kama kupasuka kwa chungu ambacho kimepasuliwa vibaya sana, bila kusalia kigae cha kuchukulia moto mekoni, au kuchotea maji kisimani.” Bwana Mungu, Mtakatifu wa Israeli, asema: “Mkinirudia na kutulia mtaokolewa; kwa utulivu na kunitumainia mtapata nguvu.” Lakini nyinyi hamkutaka. Badala yake mlisema, “La! Sisi tutakimbia na farasi wenye mbio.” Sawa, mtakimbia na farasi wenye mbio, lakini farasi wa maadui zenu wana mbio zaidi. Watu wenu elfu moja watamkimbia askari mmoja adui; na askari watano maadui watawakimbizeni nyote. Mwishowe, watakaosalia watakuwa kama mlingoti wa bendera mlimani, kama alama iliyo juu ya kilima. Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu anangoja awafadhili, atainuka na kuwaonea huruma. Maana, Mwenyezi-Mungu ni Mungu atendaye haki. Heri wote wale wanaomtumainia. Enyi watu wa Siyoni, enyi watu wa Yerusalemu, hakika nyinyi hamtaomboleza tena. Kweli Mungu atawahurumia; mara tu atakaposikia kilio chenu atawaitikeni. Ingawa Bwana atawalisha taabu na kuwanywesha dhiki, yeye ndiye Mwalimu wenu na hatajificha tena; nanyi mtamwona kwa macho yenu wenyewe. Mkienda kulia au kushoto, mtasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Njia ni hii; ifuateni.” Mtavifanya haramu vinyago vyenu vya miungu vilivyopakwa fedha na sanamu zenu zilizopakwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitu najisi, mkisema, “Poteleeni mbali!” Mtakapopanda mbegu zenu, Mwenyezi-Mungu atanyesha mvua kwa wakati wake, nazo zitakua na kuwapa mavuno mengi. Mifugo yenu nayo itapata malisho kwa wingi. Mafahali na punda wenu wa kulimia watapata malisho yaliyochambuliwa vizuri na kutiwa chumvi. Wakati utakapofika ambapo maadui watauawa na ngome zao kubomolewa, vijito vya maji vitatiririka kutoka kila mlima na kilima. Tena mwezi utawaka kama jua, nao mwanga wa jua utakuwa mara saba ya mwanga wake wa kawaida, kana kwamba mwanga wa siku saba umeangaza katika siku moja. Mambo haya yote yatatukia wakati Mwenyezi-Mungu atakapoyafunga na kuyaponya majeraha aliyowaletea watu wake.

Shirikisha
Soma Isaya 30

Isaya 30:8-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Haya, nenda sasa, andika neno hili katika kibao mbele ya macho yao, lichore katika kitabu ili liwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele. Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA; wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo; tokeni katika njia, geukeni mtoke katika mapito; mkomesheni Mtakatifu wa Israeli mbele yetu. Basi kwa ajili ya hayo Mtakatifu wa Israeli asema hivi, Kwa sababu mwalidharau neno hili, na kutumainia jeuri na ukaidi, na kuyategemea hayo; basi, uovu huu utakuwa kwenu kama mahali palipobomoka, kuanguka patokezapo katika ukuta mrefu, ambapo kuvunjika kwake huja ghafla kwa mara moja. Naye atapavunja kama chombo cha mfinyanzi kivunjwavyo, kinavyovunjwavunjwa kikatili, hata hakipatikani katika vipande vyake kigae kitoshacho kutwaa moto jikoni, au kuteka maji kisimani. Kwa maana Bwana MUNGU, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi, Kwa kurudi na kustarehe mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini; lakini hamkukubali. Bali ninyi mlisema, La! Maana tutakimbia juu ya farasi; basi, ni kweli, mtakimbia; tena, Sisi tutakimbia juu ya wanyama waendao upesi; basi, wale watakaowafuatia watakuwa wepesi. Elfu moja watakimbia kwa kukemewa na mtu mmoja; kwa kukemewa na watano mtakimbia; hata mtakapoachwa kama mlingoti juu ya kilele cha mlima, na kama bendera juu ya kilima. Kwa ajili ya hayo BWANA atangoja, ili awaonee huruma, na kwa ajili ya hayo atatukuzwa, ili awarehemu; kwa maana BWANA ni Mungu wa hukumu; heri wote wamngojao. Kwa maana watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu. Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto. Nanyi mtakitia najisi kifuniko cha sanamu zenu za fedha zilizochongwa, na mabamba ya sanamu zenu za dhahabu zilizoyeyushwa; utazitupilia mbali kama kitu kilicho najisi; utasema, Haya, toka hapa. Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng'ombe wako watakula katika malisho mapana. Ng'ombe pia na wanapunda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo. Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara. Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile BWANA atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha lao.

Shirikisha
Soma Isaya 30

Isaya 30:8-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Haya, enenda sasa, andika neno hili katika kibao mbele ya macho yao, lichore katika kitabu ili liwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele. Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA; wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo; tokeni katika njia, geukeni mtoke katika mapito; mkomesheni Mtakatifu wa Israeli mbele yetu. Basi kwa ajili ya hayo Mtakatifu wa Israeli asema hivi, Kwa sababu mwalidharau neno hili, na kutumainia jeuri na ukaidi, na kuyategemea hayo; basi, uovu huu utakuwa kwenu kama mahali palipobomoka, palipo tayari kuanguka patokezapo katika ukuta mrefu, ambapo kuvunjika kwake huja ghafula kwa mara moja. Naye atapavunja kama chombo cha mfinyanzi kivunjwavyo, akikivunja-vunja asiache kukivunja, hata hakipatikani katika vipande vyake kigae kitoshacho kutwaa moto jikoni, au kuteka maji kisimani. Kwa maana Bwana MUNGU, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi, Kwa kurudi na kustarehe mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini; lakini hamkukubali. Bali ninyi mlisema, La! Maana tutakimbia juu ya farasi; basi, ni kweli, mtakimbia; tena, Sisi tutakimbia juu ya wanyama waendao upesi; basi, wale watakaowafuatia watakuwa wepesi. Elfu moja watakimbia kwa kukemewa na mtu mmoja; kwa kukemewa na watano mtakimbia; hata mtakapoachwa kama mlingoti juu ya kilele cha mlima, na kama bendera juu ya kilima. Kwa ajili ya hayo BWANA atangoja, ili awaonee huruma, na kwa ajili ya hayo atatukuzwa, ili awarehemu; kwa maana BWANA ni Mungu wa hukumu; heri wote wamngojao. Kwa maana watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu. Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto. Nanyi mtakitia najisi kifuniko cha sanamu zenu za fedha zilizochongwa, na mabamba ya sanamu zenu za dhahabu zilizoyeyushwa; utazitupilia mbali kama kitu kilicho najisi; utasema, Haya, toka hapa. Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng’ombe zako watakula katika malisho mapana. Ng’ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo. Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara. Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile BWANA atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.

Shirikisha
Soma Isaya 30

Isaya 30:8-26 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Nenda sasa, liandike neno hili juu ya kibao kwa ajili yao, liandike kwenye kitabu, ili liweze kuwa shahidi milele kwa ajili ya siku zijazo. Hawa ni watu waasi, watoto wadanganyifu, watoto ambao hawataki kusikiliza mafundisho ya BWANA. Wanawaambia waonaji, “Msione maono tena!” Nako kwa manabii wanasema, “Msiendelee kutupatia maono ambayo ni ya kweli! Tuambieni mambo ya kupendeza, tabirini mambo ya uongo. Acheni njia hii, ondokeni katika mapito haya, nanyi acheni kutukabili pamoja na yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!” Kwa hiyo, hili ndilo asemalo yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa sababu mmekataa ujumbe huu, mkategemea uonevu na kutumainia udanganyifu, dhambi hii itakuwa kwenu kama ukuta mrefu, wenye ufa na wenye kubetuka, ambao unaanguka ghafula, mara moja. Utavunjika vipande vipande kama chombo cha udongo ukipasuka pasipo huruma ambapo katika vipande vyake hakuna kipande kitakachopatikana kwa kuukulia makaa kutoka jikoni au kuchotea maji kisimani.” Hili ndilo BWANA Mwenyezi, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, asemalo: “Katika kutubu na kupumzika ndio wokovu wenu, katika kutulia na kutumaini ndizo nguvu zenu, lakini hamkutaka. Mlisema, ‘Hapana, tutakimbia kwa farasi.’ Kwa hiyo mtakimbia! Mlisema, ‘Tutakimbia kwa farasi waendao kasi.’ Kwa hiyo wanaowafukuza watakwenda kasi! Watu 1,000 watakimbia kwa ajili ya kitisho cha mtu mmoja, kwa vitishio vya watu watano wote mtakimbia, hadi mtakapoachwa kama mlingoti wa bendera juu ya kilele cha mlima, kama bendera juu ya kilima.” Hata hivyo BWANA anatamani kutupatia neema, anainuka ili kuwaonyesha huruma. Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa haki. Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye! Enyi watu wa Sayuni, mnaoishi Yerusalemu, hamtalia tena. Tazameni jinsi atakavyokuwa na huruma mtakapolia kwa kumwomba msaada! Mara asikiapo, atawajibu. Ingawa Bwana huwapa chakula cha shida na maji ya taabu, walimu wenu hawatafichwa tena, kwa macho yenu wenyewe mtawaona. Mkigeuka kuume au kushoto, masikio yenu yatasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Hii ndiyo njia, ifuateni.” Kisha mtanajisi sanamu zenu zilizofunikwa kwa fedha, na vinyago vyenu vilivyofunikwa kwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitambaa vya wakati wa hedhi na kuziambia, “Haya, tokeni hapa!” Pia atawapa mvua kwa ajili ya mbegu mnazootesha ardhini, chakula kinachotoka ardhini kitakuwa kizuri sana, tena tele. Katika siku ile, ngʼombe wenu watalisha katika shamba pana la majani. Maksai na punda walimao watakula majani makavu na vyakula vilivyotengenezwa, vinavyotandazwa kwa uma na sepeto. Katika siku ile ya mauaji makuu, wakati minara itakapoanguka, vijito vya maji vitatiririka juu ya kila mlima mrefu na kila kilima kilichoinuka sana. Mwezi utaangaza kama jua, nao mwanga wa jua utangʼaa mara saba zaidi, kama nuru ya siku saba, wakati BWANA atakapoyafunga majeraha ya watu wake na kuwaponya vidonda alivyowatia.

Shirikisha
Soma Isaya 30