Isaya 30:8-26
Isaya 30:8-26 NEN
Nenda sasa, liandike neno hili juu ya kibao kwa ajili yao, liandike kwenye kitabu, ili liweze kuwa shahidi milele kwa ajili ya siku zijazo. Hawa ni watu waasi, watoto wadanganyifu, watoto ambao hawataki kusikiliza mafundisho ya BWANA. Wanawaambia waonaji, “Msione maono tena!” Nako kwa manabii wanasema, “Msiendelee kutupatia maono ambayo ni ya kweli! Tuambieni mambo ya kupendeza, tabirini mambo ya uongo. Acheni njia hii, ondokeni katika mapito haya, nanyi acheni kutukabili pamoja na yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!” Kwa hiyo, hili ndilo asemalo yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa sababu mmekataa ujumbe huu, mkategemea uonevu na kutumainia udanganyifu, dhambi hii itakuwa kwenu kama ukuta mrefu, wenye ufa na wenye kubetuka, ambao unaanguka ghafula, mara moja. Utavunjika vipande vipande kama chombo cha udongo ukipasuka pasipo huruma ambapo katika vipande vyake hakuna kipande kitakachopatikana kwa kuukulia makaa kutoka jikoni au kuchotea maji kisimani.” Hili ndilo BWANA Mwenyezi, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, asemalo: “Katika kutubu na kupumzika ndio wokovu wenu, katika kutulia na kutumaini ndizo nguvu zenu, lakini hamkutaka. Mlisema, ‘Hapana, tutakimbia kwa farasi.’ Kwa hiyo mtakimbia! Mlisema, ‘Tutakimbia kwa farasi waendao kasi.’ Kwa hiyo wanaowafukuza watakwenda kasi! Watu 1,000 watakimbia kwa ajili ya kitisho cha mtu mmoja, kwa vitishio vya watu watano wote mtakimbia, hadi mtakapoachwa kama mlingoti wa bendera juu ya kilele cha mlima, kama bendera juu ya kilima.” Hata hivyo BWANA anatamani kutupatia neema, anainuka ili kuwaonyesha huruma. Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa haki. Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye! Enyi watu wa Sayuni, mnaoishi Yerusalemu, hamtalia tena. Tazameni jinsi atakavyokuwa na huruma mtakapolia kwa kumwomba msaada! Mara asikiapo, atawajibu. Ingawa Bwana huwapa chakula cha shida na maji ya taabu, walimu wenu hawatafichwa tena, kwa macho yenu wenyewe mtawaona. Mkigeuka kuume au kushoto, masikio yenu yatasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Hii ndiyo njia, ifuateni.” Kisha mtanajisi sanamu zenu zilizofunikwa kwa fedha, na vinyago vyenu vilivyofunikwa kwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitambaa vya wakati wa hedhi na kuziambia, “Haya, tokeni hapa!” Pia atawapa mvua kwa ajili ya mbegu mnazootesha ardhini, chakula kinachotoka ardhini kitakuwa kizuri sana, tena tele. Katika siku ile, ngʼombe wenu watalisha katika shamba pana la majani. Maksai na punda walimao watakula majani makavu na vyakula vilivyotengenezwa, vinavyotandazwa kwa uma na sepeto. Katika siku ile ya mauaji makuu, wakati minara itakapoanguka, vijito vya maji vitatiririka juu ya kila mlima mrefu na kila kilima kilichoinuka sana. Mwezi utaangaza kama jua, nao mwanga wa jua utangʼaa mara saba zaidi, kama nuru ya siku saba, wakati BWANA atakapoyafunga majeraha ya watu wake na kuwaponya vidonda alivyowatia.