Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwa 24:28-49

Mwa 24:28-49 SUV

Basi yule msichana akapiga mbio, akawaambia watu wa nyumba ya mama yake mambo hayo. Na Rebeka alikuwa na kaka, jina lake Labani. Labani akatoka mbio kumwendea yule mtu kisimani. Ikawa, alipoiona ile pete, na vikuku mikononi mwa nduguye, akasikia maneno ya Rebeka nduguye, akisema, Hivyo ndivyo alivyoniambia mtu huyo, basi akamjia mtu yule, na tazama, amesimama karibu na ngamia kisimani. Akasema, Karibu, wewe uliyebarikiwa na BWANA, mbona unasimama nje? Kwa maana nimeiweka nyumba tayari, na nafasi kwa ngamia. Na mtu yule akaingia katika nyumba, akawafungua ngamia; naye akatoa majani na malisho kwa ngamia, na maji ya kuoshea miguu yake, na miguu ya watu waliokuwa pamoja naye. Akaandaliwa chakula, lakini akasema, Sili mpaka niseme kwanza maneno yangu. Akamwambia, Haya, sema. Akasema, Mimi ni mtumwa wa Ibrahimu, na BWANA amembarikia sana bwana wangu, amekuwa mtu mkuu; amempa kondoo, na ng’ombe, na fedha, na dhahabu, na watumwa, na wajakazi, na ngamia, na punda. Naye Sara, mkewe bwana wangu, akamzalia bwana wangu mwana wa kiume, katika uzee wake; naye amempa yote aliyo nayo. Kisha bwana wangu akaniapisha akisema, Usimtwalie mwanangu mke wa binti za Wakanaani, ambao nakaa katika nchi yao. Ila uende mpaka nyumbani kwa babangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu mke. Nikamwambia bwana wangu, Labda huyo mwanamke hatafuatana nami. Akaniambia, BWANA, ambaye naenenda machoni pake, atapeleka malaika wake pamoja nawe, atafanikisha njia yako; nawe umtwalie mwanangu mke katika jamaa zangu, na wa nyumba ya babangu. Ndipo utafunguliwa kiapo changu hapo utakapowafikilia jamaa zangu; nao wasipokupa msichana huyo, utafunguliwa kiapo changu. Nami nikaja leo kisimani, nikasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ukinifanikishia sasa njia yangu niendayo mimi, tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji; basi na iwe hivi, msichana ajaye kuteka maji, nikamwambia, Nipe, nakuomba, maji kidogo katika mtungi wako ninywe, naye akaniambia, Unywe wewe, na ngamia zako pia nitawatekea, huyo na awe ndiye mke BWANA aliyemwekea mwana wa bwana wangu. Hata kabla sijaisha kusema moyoni mwangu, tazama! Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka. Nami nikamwambia, Tafadhali nipe maji ninywe. Akafanya haraka akatua mtungi wake chini, akanena, Unywe, na ngamia zako nitawanywesha pia; basi nikanywa, akawanywesha na ngamia nao. Kisha nikamwuliza nikasema, U binti wa nani wewe? Naye akasema, Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia. Nami nikamtia hazama puani mwake na vikuku mikononi mwake. Nikainama, nikamsujudia BWANA, nikamtukuza BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, aliyeniongoza njiani, nimtwalie mwana wa bwana wangu binti wa ndugu yake. Basi, kama mnataka kumfanyia rehema na kweli bwana wangu, niambieni kama sivyo, niambieni; ili nigeuke upande wa kuume au wa kushoto.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwa 24:28-49