Mwanzo 24:28-49
Mwanzo 24:28-49 NEN
Yule msichana akakimbia akawaeleza watu wa nyumbani mwa mama yake kuhusu mambo haya. Rebeka alikuwa na kaka aliyeitwa Labani, huyo akaharakisha kukutana na yule mtumishi kule kisimani. Mara alipoiona ile pete puani, na bangili mikononi mwa dada yake na kusikia yale maneno Rebeka aliyoambiwa na huyo mtumishi, alimwendea huyo mtumishi, akamkuta amesimama karibu na ngamia wake pale karibu na kisima. Akamwambia, “Karibu nyumbani wewe uliyebarikiwa na BWANA, kwa nini unasimama huko nje? Mimi nimekuandalia nyumba na mahali kwa ajili ya ngamia.” Hivyo yule mtumishi akaenda nyumbani, mizigo ikaondolewa juu ya ngamia. Majani na malisho yakaletwa kwa ajili ya ngamia na maji kwa ajili yake na watu wake ili kunawa miguu. Ndipo chakula kikaandaliwa kwa ajili yake, lakini akasema, “Sitakula mpaka niwe nimewaambia yale niliyo nayo ya kusema.” Labani akasema, “Basi tuambie.” Hivyo akasema, “Mimi ni mtumishi wa Abrahamu. BWANA amembariki sana bwana wangu, amekuwa tajiri. Amempa kondoo na ngʼombe, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda. Sara mkewe bwana wangu amemzalia mwana katika uzee wake, naye amempa kila kitu alichokuwa nacho. Naye bwana wangu ameniapisha na akasema, ‘Kamwe usimtwalie mwanangu mke katika binti za Wakanaani, ambao ninaishi katika nchi yao, ila uende mpaka kwa jamaa ya baba yangu na ukoo wangu mwenyewe, ukamtwalie mwanangu mke huko.’ “Kisha nikamuuliza bwana wangu, ‘Je, kama huyo mwanamke hatakubali kurudi nami?’ “Akanijibu, ‘BWANA ambaye nimetembea mbele zake, atatuma malaika wake pamoja nawe, na kuifanikisha safari yako, ili uweze kupata mke kwa ajili ya mwanangu katika ukoo wangu na kutoka jamaa ya baba yangu. Kisha, utakapokwenda kwenye ukoo wangu, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu hata kama wakikataa kukupa huyo binti, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu.’ “Nilipokuja kisimani leo nilisema, ‘Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ikikupendeza, naomba uifanikishe safari niliyoijia. Tazama, ninasimama kando ya kisima hiki, kama mwanamwali akija kuteka maji nami nikimwambia, tafadhali niruhusu ninywe maji kidogo kutoka kwenye mtungi wako, naye kama akiniambia, “Kunywa, nami nitateka maji kwa ajili ya ngamia wako pia,” basi huyo awe ndiye mke ambaye BWANA amemchagulia mwana wa bwana wangu.’ “Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, Rebeka akatokea, amebeba mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka maji, nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ninywe.’ “Akafanya haraka kushusha mtungi wake begani na kusema, ‘Kunywa na nitawanywesha ngamia wako pia,’ basi nikanywa, akawanywesha na ngamia pia. “Nikamuuliza, ‘Wewe ni binti wa nani?’ “Akasema, ‘Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia.’ “Ndipo nilipotia pete puani mwake na bangili mikononi mwake, nikasujudu na nikamwabudu BWANA. Nikamtukuza BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, aliyeniongoza katika njia sahihi ili nimtwalie mwana na bwana wangu mke katika jamaa zake. Ikiwa mtaonyesha wema na uaminifu kwa bwana wangu, mniambie, la sivyo, mniambie, ili niweze kujua njia ya kugeukia.”