Ezr 8:24-36
Ezr 8:24-36 SUV
Ndipo nikawatenga watu kumi na wawili wa wakuu wa makuhani, nao ni Sherebia, na Hashabia, na watu kumi wa ndugu zao pamoja nao, nami nikawapimia kwa mizani zile fedha, na dhahabu, na vile vyombo, matoleo kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu, ambayo mfalme, na washauri wake, na wakuu wake, na Israeli wote waliokuwapo, walikuwa wameyatoa; nami nikawapimia mikononi mwao talanta za fedha mia sita na hamsini na vyombo vya fedha talanta mia; na talanta mia za dhahabu; na mabakuli ishirini ya dhahabu, thamani yake darkoni elfu; na vyombo viwili vya shaba nzuri iliyong’aa, thamani yake sawa na dhahabu. Kisha nikawaambia, Ninyi mmekuwa watakatifu kwa BWANA, na hivyo vyombo ni vitakatifu; na fedha na dhahabu ni matoleo ya hiari kwa BWANA, Mungu wa baba zenu. Basi, angalieni, na kuvitunza vitu hivi, hata mtakapovipima mbele ya wakuu wa makuhani, na Walawi, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli, huko Yerusalemu, katika vyumba vya nyumba ya BWANA. Hivyo makuhani na Walawi wakaupokea uzani wa fedha, na dhahabu, na vyombo, ili kuvileta Yerusalemu nyumbani kwa Mungu wetu. Ndipo tukasafiri toka mtoni Ahava siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza, ili kwenda Yerusalemu; na mkono wa Mungu ulikuwa pamoja nasi, akatuokoa na mkono wa adui, na mtu mwenye kutuvizia njiani. Tukafika Yerusalemu, tukakaa huko muda wa siku tatu. Hata siku ya nne, hizo fedha na dhahabu na vile vyombo vilipimwa ndani ya nyumba ya Mungu, vikatiwa mikononi mwa Meremothi, mwana wa Uria, kuhani; na pamoja naye alikuwapo Eleazari, mwana wa Finehasi; na pamoja nao Yozabadi, mwana wa Yeshua, na Noadia, mwana wa Binui, Walawi; vile vyombo vyote kwa hesabu na kwa uzani; tena uzani wake wote uliandikwa wakati ule. Na wana wa uhamisho, waliokuwa wametoka katika uhamisho wakamtolea Mungu wa Israeli sadaka za kuteketezwa, ng’ombe kumi na wawili kwa ajili ya Israeli wote, na kondoo waume tisini na sita, na wana-kondoo sabini na saba, na mbuzi waume kumi na wawili, kuwa sadaka ya dhambi, hao wote pia walikuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA. Wakawapa manaibu wa mfalme, na maliwali wa ng’ambo ya Mto, maagizo ya mfalme; nao wakawapa watu, na nyumba ya Mungu, msaada.