Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 8:24-36

Ezra 8:24-36 NENO

Kisha niliwatenga viongozi wa makuhani kumi na wawili, pamoja na Sherebia, Hashabia na ndugu zao kumi, nami nikawapimia fedha, dhahabu na vifaa ambavyo mfalme, washauri wake, maafisa wake na Waisraeli wote waliokuwepo walikuwa wamevitoa sadaka kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu. Niliwapimia talanta mia sita na hamsini za fedha, vifaa vingine vya fedha vya uzito wa talanta mia moja, talanta mia moja za dhahabu, mabakuli ishirini ya dhahabu ya thamani ya darkoni elfu moja, na vyombo viwili vya shaba iliyosuguliwa, ya thamani kama dhahabu. Niliwaambia, “Ninyi pamoja na vyombo hivi ni wakfu kwa Mwenyezi Mungu. Fedha na dhahabu ni sadaka ya hiari kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu. Vilindeni kwa uangalifu hadi mtakapovipima ndani ya vyumba vya nyumba ya Mwenyezi Mungu katika Yerusalemu mbele ya makuhani, viongozi na Walawi pamoja na wakuu wa jamaa za Israeli.” Ndipo makuhani na Walawi wakapokea fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu ambavyo vilipimwa na kupelekwa katika nyumba ya Mungu wetu mjini Yerusalemu. Tulianza safari kutoka Mto Ahava kwenda Yerusalemu siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza. Mkono wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, naye njiani alitulinda dhidi ya adui na wanyang’anyi. Kwa hiyo tuliwasili Yerusalemu ambapo tulipumzika kwa siku tatu. Katika siku ya nne, ndani ya nyumba ya Mungu wetu, tulipima fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu, tukakabidhi mikononi mwa kuhani Meremothi mwana wa Uria. Eleazari mwana wa Finehasi alikuwa pamoja naye, na pia Walawi wawili, Yozabadi mwana wa Yeshua, na Noadia mwana wa Binui. Kila kitu kilihesabiwa kwa idadi na kupimwa kwa uzito, nao uzito wote uliandikwa wakati ule. Kisha mateka waliokuwa wamerudi kutoka utumwani wakatoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Mungu wa Israeli: mafahali kumi na wawili kwa ajili ya Israeli wote, kondoo dume tisini na sita, wana-kondoo sabini na saba, na beberu kumi na wawili kuwa sadaka ya dhambi. Hii yote ilikuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu. Pia walikabidhi manaibu wa mfalme na watawala wa Ng’ambo ya Mto Frati maagizo ya mfalme, ambao baadaye walitoa msaada kwa watu na kwa nyumba ya Mungu.