Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezr 8:15-23

Ezr 8:15-23 SUV

Nikawakusanya penye mto ushukao kwenda Ahava; na huko tukapiga kambi yetu muda wa siku tatu; nikawakagua watu, na makuhani, wala sikuona hapo wana wa Lawi hata mmoja. Ndipo nikatuma watu kwenda kumwita Eliezeri, na Arieli, na Shemaya, na Elnathani, na Yaribu, na Elnathani, na Nathani, na Zekaria, na Meshulamu, waliokuwa wakuu; na Yoyaribu, na Elnathani pia, waliokuwa waalimu. Nikawapeleka kwa Ido, mkuu, huko Kasifia; nikawaambia watakayomwambia Ido, na ndugu zake hao Wanethini, huko Kasifia, kwamba watuletee watu watakaohudumu katika nyumba ya Mungu wetu. Na kama mkono mwema wa Mungu wetu ulivyokuwa pamoja nasi, wakamletea Ishekeli, mmoja wa wana wa Mali, mwana wa Lawi, mwana wa Israeli; na Sherebia, pamoja na wanawe na ndugu zake, watu kumi na wanane; na Hashabia, na pamoja naye Yeshaya, wa wana wa Merari, na ndugu zake na wana wao, watu ishirini; na katika Wanethini, ambao Daudi, na wakuu, walikuwa wamewaweka kwa ajili ya utumishi wa Walawi, Wanethini mia mbili na ishirini; wote wametajwa kwa majina yao. Ndipo nikaamuru kufunga, hapo penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za Mungu, na kutafuta kwake njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe, na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote. Maana naliona haya kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapanda farasi, ili kutusaidia juu ya adui njiani; kwa maana tulikuwa tumesema na mfalme, tukinena, Mkono wa Mungu u juu ya watu wote wamtafutao, kuwatendea mema; bali uweza wake na ghadhabu yake ni kinyume cha wote wamwachao. Basi tukafunga, tukamsihi Mungu wetu kwa ajili ya hayo; naye akatutakabali.