Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 8:15-23

Ezra 8:15-23 NENO

Niliwakusanya kwenye mto unaotiririka kuelekea Ahava, nasi tukapiga kambi pale siku tatu. Nilipokagua kati ya watu na makuhani, sikuwapata Walawi. Basi niliwaita Eliezeri, Arieli, Shemaya, Elnathani, Yaribu, Elnathani, Nathani, Zekaria na Meshulamu waliokuwa viongozi na Yoyaribu na Elnathani waliokuwa wasomi, nikawatuma kwa Ido kiongozi huko Kasifia. Niliwaambia watakayomwambia Ido na ndugu zake, watumishi wa Hekalu huko Kasifia, ili waweze kutuletea wahudumu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu. Kwa sababu mkono wa neema wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, walituletea Sherebia, mtu mwenye busara kutoka wazao wa Mahli mwana wa Lawi, mwana wa Israeli, na wana wa Sherebia pamoja na ndugu zao wanaume kumi na nane. Naye Hashabia, pamoja na Yeshaya kutoka wazao wa Merari na ndugu zake na wapwa wake, walikuwa wanaume ishirini. Vilevile walileta watumishi wa Hekalu mia mbili na ishirini, kikundi ambacho Daudi na maafisa walikuwa wamekianzisha ili kusaidia Walawi. Wote waliorodheshwa kwa majina. Kando ya Mto Ahava, hapo nilitangaza kufunga, ili tujinyenyekeze mbele za Mungu wetu na kumwomba kwa ajili ya kutujalia safari ya amani sisi na watoto wetu, pamoja na mali yetu yote. Niliona aibu kumwomba mfalme askari na wapanda farasi wa kutulinda njiani kutokana na adui zetu, kwa sababu tulikwisha kumwambia mfalme, “Mkono wa neema wa Mungu wetu uko juu ya kila mmoja anayemtafuta, lakini hasira yake kubwa ni dhidi ya wote wamwachao.” Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu wetu kuhusu jambo hili, naye akajibu maombi yetu.