Kut 40:17-33
Kut 40:17-33 SUV
Hata mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili, siku ya kwanza ya mwezi ile maskani ilisimamishwa. Musa akaisimamisha maskani, akayaweka matako yake, akazisimamisha mbao zake akayatia mataruma yake, akazisimamisha nguzo zake. Akaitanda hema juu ya maskani, akakitia kifuniko cha hema juu yake; kama BWANA alivyomwamuru Musa. Akautwaa ule ushuhuda, akautia ndani ya sanduku, akaiweka miti ya kuchukulia juu ya sanduku, akakiweka kiti cha rehema juu ya sanduku; kisha akalileta sanduku akalitia ndani ya maskani, naye akalitundika pazia la sitara, akalisitiri sanduku la ushuhuda; kama BWANA alivyomwamuru Musa. Akaitia meza ndani ya hema ya kukutania, upande wa maskani ulioelekea kaskazini, nje ya pazia. Akaipanga ile mikate juu yake mbele za BWANA; kama BWANA alivyomwamuru Musa. Kisha akakitia kinara cha taa ndani ya hema ya kukutania, kuikabili ile meza, upande wa maskani ulioelekea kusini. Kisha akaziwasha taa zake mbele za BWANA, kama BWANA alivyomwamuru Musa. Akaitia madhabahu ya dhahabu ndani ya hema ya kukutania mbele ya pazia. Akafukiza juu yake uvumba wa manukato kama BWANA alivyomwamuru Musa. Akalitia pazia la mlango wa maskani. Akaiweka madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mlangoni pa maskani ya kukutania, akatoa sadaka ya kuteketezwa juu yake, na sadaka ya unga; kama BWANA alivyomwamuru Musa. Akaliweka birika kati ya hema ya kukutania na madhabahu, akatia maji ndani yake ya kuoshea. Musa na Haruni, na wanawe wakanawa mikono yao na miguu yao ndani yake; hapo walipoingia hema ya kukutania, na hapo walipoikaribia madhabahu walinawa kama BWANA alivyomwamuru Musa. Akausimamisha ukuta wa ua kuizunguka maskani na madhabahu, akalitundika pazia la mlango wa ule ua. Basi Musa akaimaliza hiyo kazi.