Kut 35:1-19
Kut 35:1-19 SUV
Musa akakutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli, na kuwaambia, Maneno aliyoyausia BWANA ni haya, kwamba myafanye. Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa BWANA; mtu awaye yote atakayefanya kazi yo yote katika siku hiyo atauawa. Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku ya Sabato. Kisha Musa akanena na mkutano wote wa wana wa Israeli, akawaambia, Neno hili ndilo aliloliamuru BWANA, akisema, Katwaeni kati yenu matoleo kwa BWANA; mtu awaye yote aliye na moyo wa kupenda, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba; na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri, na singa za mbuzi; na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, na mbao za mshita; na mafuta kwa hiyo taa, na viungo vya manukato kwa hayo mafuta ya kutiwa, na kwa huo uvumba mzuri; na vito vya shohamu, na vito vya kutiwa kwa hiyo naivera, na kwa hicho kifuko cha kifuani. Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa hekima na aje, na kuyafanya hayo yote ambayo BWANA ameyaagiza; yaani, hiyo maskani na hema yake, na kifuniko chake, na vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na viguzo vyake, na matako yake; hilo sanduku, na miti yake, na hicho kiti cha rehema, na lile pazia la sitara; na hiyo meza, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hiyo mikate ya wonyesho; na hicho kinara cha taa kwa mwanga, na vyombo vyake, na taa zake, na hayo mafuta kwa nuru; na hiyo madhabahu ya kufukizia uvumba, na miti yake, na hayo mafuta ya kupaka, na huo uvumba mzuri, na hicho kisitiri cha mlango, mlangoni mwa hiyo maskani; na hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, pamoja na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hilo birika na tako lake; na hizo kuta za nguo za ua, na viguzo vyake, na matako yake, na pazia la lango la ua; na vile vigingi vya maskani, na vigingi vya ua, na kamba zake na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, kwa ajili ya kutumika ndani ya mahali patakatifu, hayo mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.