Kutoka 35:1-19
Kutoka 35:1-19 NEN
Mose akakusanya jumuiya yote ya Waisraeli na kuwaambia, “Haya ndiyo mambo ambayo BWANA amewaamuru ninyi mfanye: Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba itakuwa takatifu kwenu, Sabato ya kupumzika kwa BWANA. Yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo ni lazima auawe. Msiwashe moto mahali popote katika makazi yenu siku ya Sabato.” Mose akaiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Hili ndilo BWANA aliloamuru: Toeni sadaka kwa BWANA kutoka mali mliyo nayo. Kila mmoja aliye na moyo wa kupenda atamletea BWANA sadaka ya dhahabu, fedha na shaba; nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi; singa za mbuzi; ngozi za kondoo dume zilizopakwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo; mbao za mshita; mafuta ya zeituni kwa ajili ya taa; vikolezi kwa ajili ya mafuta ya upako, pamoja na uvumba wa harufu nzuri; vito vya shohamu, na vito vingine vya thamani vya kuweka kwenye kisibau na kile kifuko cha kifuani. “Wote wenye ujuzi miongoni mwenu inawapasa kuja na kutengeneza kila kitu BWANA alichoamuru: Maskani pamoja na hema lake na kifuniko chake, vibanio, mihimili, mataruma, nguzo na vitako; Sanduku la Agano pamoja na mipiko yake, kifuniko cha kiti cha rehema na pazia linalokizuia; meza na mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, mikate ya Wonyesho; kinara cha taa kwa ajili ya mwanga pamoja na vifaa vyake vyote, taa na mafuta kwa ajili ya mwanga; madhabahu ya kufukiza uvumba pamoja na mipiko yake, mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri; pazia la mlangoni mahali pa kuingilia ndani ya maskani; madhabahu ya sadaka za kuteketeza pamoja na wavu wake wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote; sinia la shaba pamoja na tako lake; pazia la eneo la ua pamoja na nguzo zake na vitako vyake, pazia la ingilio la kwenye ua; vigingi vya hema kwa ajili ya maskani pamoja na ua na kamba zake; mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa wakati wa huduma katika mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu kwa ajili ya kuhani Aroni, na mavazi kwa ajili ya wanawe watakapokuwa wakihudumu katika kazi ya ukuhani.”