Kut 26:1-14
Kut 26:1-14 SUV
Kisha fanya hiyo maskani iwe na mapazia kumi; ifanye ya nguo ya kitani nzuri ya kusokota, pamoja na nyuzi za rangi ya samawi, na ya zambarau, na nyekundu, pamoja na makerubi; kazi ya fundi stadi. Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa ishirini na nane, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne; mapazia yote yatakuwa ya kipimo kimoja. Mapazia matano yataungwa pamoja, hili na hili; na mapazia matano mengine yataungwa pamoja, hili na hili. Kisha utafanya tanzi za rangi ya samawi upande wa mwisho wa pazia moja katika ule upindo wa fungu lake, vivyo utafanya upande wa mwisho wa ile pazia iliyo, katika fungu la pili. Fanya matanzi hamsini katika pazia moja, na matanzi hamsini katika upande wa mwisho wa ile pazia iliyo katika kuungana kwa pili; hizo tanzi zitaelekeana. Kisha ufanye vifungo hamsini vya dhahabu, na kuunganya hayo mapazia pamoja kwa vile vifungo; na hiyo maskani itakuwa ni moja. Nawe fanya mapazia ya singa za mbuzi yawe hema juu ya maskani; fanya mapazia kumi na moja. Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa thelathini, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne; hayo mapazia kumi na moja yatakuwa ya kipimo kimoja. Kisha utaunganya mapazia matano mbali, na mapazia sita mbali, na lile pazia la sita utalipeta hapo upande wa mbele wa ile hema. Fanya tanzi hamsini upande wa mwisho wa pazia lile lililo la mwisho katika hayo yaliyounganywa pamoja, na tanzi hamsini upande wa mwisho wa lile pazia lililo nje katika hayo ya pili yaliyounganywa pamoja. Tena ufanye vifungo hamsini vya shaba, na kuvitia vile vifungo katika zile tanzi, na kuiunganya ile hema pamoja, ili iwe hema moja. Na kipande kile kilichosalia, kile kiangukacho, cha yale mapazia ya hema, ile nusu ya pazia iliyosalia, itaanguka huko upande wa nyuma wa maskani. Na hiyo dhiraa moja upande mmoja, na ile dhiraa moja upande wa pili, ya urefu wa mapazia ya hema uliosalia, zitaanguka katika ubavu wa maskani upande huu na upande huu, ili kuifunika. Nawe fanya kifuniko cha ile hema, cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo.