Kum 4:1-14
Kum 4:1-14 SUV
Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za BWANA, Mungu wenu, niwaamuruzo. Macho yenu yameona aliyoyatenda BWANA kwa sababu ya Baal-peori; maana wote waliomfuata Baal-peori, BWANA, Mungu wako, amewaangamiza kutoka kati yako. Bali ninyi mlioambatana na BWANA, Mungu wenu, mnaishi kila mmoja wenu, hata leo. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama BWANA, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako; siku ile uliyosimama mbele za BWANA wako huko Horebu, BWANA aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, wakapate na kuwafundisha watoto wao. Mkakaribia, mkasimama chini ya ule mlima; mlima ukawaka moto mpaka kati ya mbinguni, kwa giza na mawingu, na giza kuu. BWANA akasema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lo lote; sauti tu. Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za mawe. BWANA akaniamuru wakati ule niwafundishe maagizo na hukumu, mpate kuzitenda katika nchi ile mtakayoivukia ili kuimiliki.