Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 4:1-14

Kumbukumbu la Sheria 4:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Mose akaendelea kusema, “Zingatieni basi na kufuata masharti yote na maagizo niliyowafundisha, ili mpate kuishi na kumiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, anawapeni. Msiongeze chochote katika amri ninazowapeni, wala msipunguze kitu; zingatieni amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambazo ninawapeni. Nyinyi mliona kwa macho yenu mambo ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafanya kuhusu Baal-peori. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwaangamiza watu wote miongoni mwenu waliomwabudu huyo mungu Baal-peori. Lakini nyinyi mliokuwa waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mko hai hadi leo. “Haya! Nimewafundisheni masharti na maagizo kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, alivyoniamuru nifanye, ili muyazingatie katika nchi mnayokwenda kuimiliki. Shikeni na kuyatekeleza masharti na maagizo hayo maana mkifanya hivyo watu wa mataifa mengine watakapopata kujua masharti hayo, watatambua kuwa nyinyi ni wenye hekima na busara, wakisema: ‘Kweli watu wa taifa hili kuu wana hekima na busara!’ “Hakuna taifa lolote hata liwe kuu namna gani, ambalo mungu wake yuko karibu nalo, kama alivyo karibu nasi Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, tunapomwomba msaada. Wala hakuna taifa lingine lolote hata liwe kuu namna gani, lenye masharti na maagizo ya haki, kama hayo ambayo nimewafundisha siku hii ya leo. “Lakini muwe waangalifu na kujihadhari sana msije mkasahau mambo yale mliyoyaona kwa macho yenu wenyewe. Isije ikatokea hata mara moja maishani mwenu mambo hayo yakasahaulika mioyoni mwenu. Wasimulieni watoto wenu na wajukuu wenu juu ya siku ile ambayo mlisimama mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kule Horebu, aliponiambia, ‘Wakusanye hao watu mbele yangu, niwaambie maneno yangu ili wajifunze kunicha mimi siku zote za maisha yao, na kuwafundisha watoto wao kufanya hivyo’. “Basi, mlikaribia na kusimama chini ya ule mlima ambao wakati huo ulikuwa unawaka moto uliofika mpaka mbinguni ukiwa umetanda giza na wingu zito. Kisha Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi kutoka katikati ya moto huo; mliyasikia maneno aliyosema lakini hamkumwona; mlisikia tu sauti yake. Naye akawatangazia agano lake akawaamuru mlishike yaani mzitii zile amri kumi ambazo aliziandika juu ya vibao viwili vya mawe. Wakati huo Mwenyezi-Mungu aliniamuru niwafundishe masharti na maagizo yote ambayo mnapaswa kuyatekeleza katika nchi mnayokwenda kuimiliki.

Kumbukumbu la Sheria 4:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu ninazowafundisha, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi anayowapa BWANA, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno ninalowaamuru wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za BWANA, Mungu wenu, ninazowaamuru. Macho yenu yameona aliyoyatenda BWANA kwa sababu ya Baal-peori; maana wote waliomfuata Baal-peori, BWANA, Mungu wako, amewaangamiza kutoka kati yako. Bali ninyi mlioambatana na BWANA, Mungu wenu, mnaishi kila mmoja wenu, hata leo. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama BWANA, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA Mungu wetu alivyo kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo? Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako; siku ile uliyosimama mbele za BWANA wako huko Horebu, BWANA aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawafanya wasikilize maneno yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, wakapate na kuwafundisha watoto wao. Mkakaribia, mkasimama chini ya ule mlima; mlima ukawaka moto mpaka kati ya mbinguni, kwa giza na mawingu, na giza kuu. BWANA akasema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lolote; sauti tu. Akawahubiria agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika katika vibao viwili vya mawe. BWANA akaniamuru wakati ule niwafundishe maagizo na hukumu, mpate kuzitenda katika nchi ile mtakayoivukia ili kuimiliki.

Kumbukumbu la Sheria 4:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za BWANA, Mungu wenu, niwaamuruzo. Macho yenu yameona aliyoyatenda BWANA kwa sababu ya Baal-peori; maana wote waliomfuata Baal-peori, BWANA, Mungu wako, amewaangamiza kutoka kati yako. Bali ninyi mlioambatana na BWANA, Mungu wenu, mnaishi kila mmoja wenu, hata leo. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama BWANA, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako; siku ile uliyosimama mbele za BWANA wako huko Horebu, BWANA aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, wakapate na kuwafundisha watoto wao. Mkakaribia, mkasimama chini ya ule mlima; mlima ukawaka moto mpaka kati ya mbinguni, kwa giza na mawingu, na giza kuu. BWANA akasema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lo lote; sauti tu. Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za mawe. BWANA akaniamuru wakati ule niwafundishe maagizo na hukumu, mpate kuzitenda katika nchi ile mtakayoivukia ili kuimiliki.

Kumbukumbu la Sheria 4:1-14 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Sikia sasa, ee Israeli, amri na sheria nitakazokufundisha wewe. Zifuate ili upate kuishi na uingie kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zako, anawapa. Usiongeze wala usipunguze chochote ninachowaamuru ninyi, ila myashike maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambayo nawapa. Mliona kwa macho yenu wenyewe kile Mwenyezi Mungu alichokifanya kule Baal-Peori. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwaangamiza kutoka miongoni mwenu kila mmoja aliyemfuata Baali wa Peori, lakini ninyi nyote mlioshikamana na Mwenyezi Mungu kwa uthabiti, Mungu wenu, mko hai hadi leo. Tazama, nimewafundisha amri na sheria kama Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, alivyoniamuru mimi, ili mzifuate katika nchi mnayoiingia kuimiliki. Zishikeni kwa uangalifu, kwa kuwa hii itaonesha hekima na ufahamu wenu kwa mataifa, ambayo yatasikia kuhusu amri zote hizi, nao watasema, “Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na ufahamu.” Ni taifa gani jingine lililo kubwa kiasi cha kuwa na miungu yao iliyo karibu nao kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alivyo karibu nasi wakati wowote tunapomwomba? Nalo ni taifa gani jingine lililo kubwa hivi lenye kuwa na amri na sheria za haki kama hizi ninazoweka mbele yenu leo? Mwe waangalifu na makini ili msije mkasahau mambo ambayo mliyaona kwa macho yenu, wala kuyaacha yaondoke mioyoni mwenu siku zote za uhai wenu. Mwafundishe hayo watoto wenu na watoto wao baada yao. Kumbuka siku uliyosimama mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kule Horebu aliponiambia, “Wakutanishe watu mbele yangu wasikie maneno yangu ili waweze kujifunza kuniheshimu kwa muda wote watakaoishi katika nchi, nao waweze kuwafundisha watoto wao maneno hayo.” Mlisogea karibu na mkasimama chini ya mlima wakati ulipowaka moto hadi juu mbinguni, pamoja na mawingu meusi na giza nene. Ndipo Mwenyezi Mungu alipozungumza nanyi kutoka kati ya moto. Mkasikia sauti ya maneno lakini hamkuona umbo, kulikuwa na sauti tu. Aliwatangazia agano lake, hizo Amri Kumi ambazo aliwaamuru mzifuate, kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe. Naye Mwenyezi Mungu alinielekeza wakati huo kuwafundisha ninyi sheria na amri ambazo mnapaswa kuzifuata katika nchi ambayo mnavuka Yordani kuimiliki.