Kum 32:1-14
Kum 32:1-14 SUV
Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitanena; Na nchi isikie maneno ya kinywa changu. Mafundisho yangu yatadondoka kama mvua, Maneno yangu yatatona-tona kama umande; Kama manyunyu juu ya majani mabichi; Kama matone ya mvua juu ya mimea. Maana nitalitangaza Jina la BWANA; Mpeni ukuu Mungu wetu. Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na adili. Wametenda mambo ya uharibifu, Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao; Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka. Je! Mnamlipa BWANA hivi, Enyi watu wapumbavu na ujinga? Je! Yeye siye baba yako aliyekununua? Amekufanya, na kukuweka imara. Kumbuka siku za kale, Tafakari miaka ya vizazi vingi; Mwulize baba yako, naye atakuonyesha; Wazee wako, nao watakuambia. Yeye Aliye Juu alipowapa mataifa urithi wao, Alipowabagua wanadamu, Aliweka mipaka ya watu Kwa kadiri ya hesabu ya wana wa Israeli. Maana, sehemu ya BWANA ni watu wake, Yakobo ni kura ya urithi wake. Alimkuta katika nchi ya ukame, Na katika jangwa tupu litishalo; Alimzunguka, akamtunza; Akamhifadhi kama mboni ya jicho; Mfano wa tai ataharikishaye kioto chake; Na kupapatika juu ya makinda yake, Alikunjua mbawa zake, akawatwaa, Akawachukua juu ya mbawa zake; BWANA peke yake alimwongoza, Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye. Alimpandisha mahali pa nchi palipoinuka, Naye akala mazao ya mashamba; Akamnyonyesha asali iliyotoka jabalini, Na mafuta yaliyotoka katika mwamba wa gumegume; Siagi ya ng’ombe, na maziwa ya kondoo, Pamoja na mafuta ya wana-kondoo, Kondoo waume wa Kibashani, na mbuzi, Na unono wa ngano iliyo nzuri; Ukanywa divai, damu ya mizabibu.