Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 32:1-14

Kumbukumbu 32:1-14 NEN

Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitasema; sikia, ee nchi, maneno ya kinywa changu. Mafundisho yangu na yanyeshe kama mvua, na maneno yangu na yashuke kama umande, kama manyunyu juu ya majani mabichi, kama mvua tele juu ya mimea myororo. Nitalitangaza jina la BWANA. Naam, sifuni ukuu wa Mungu wetu! Yeye ni Mwamba, kazi zake ni kamilifu, njia zake zote ni haki. Mungu mwaminifu ambaye hakosei, yeye ni mnyofu na mwenye haki. Wamefanya mambo ya upotovu mbele zake; kwa aibu yao, wao si watoto wake tena, lakini ni kizazi kilicho kiovu na kilichopotoka. Je, hii ndiyo njia ya kumlipa BWANA, enyi watu wajinga na wasio na busara? Je, yeye siye Baba yenu, Muumba wenu, aliyewafanya ninyi na kuwaumba? Kumbuka siku za kale; tafakari vizazi vya zamani vilivyopita. Uliza baba yako, naye atakuambia, wazee wako, nao watakueleza. Aliye Juu Sana alipowapa mataifa urithi wao, alipogawanya wanadamu wote, aliweka mipaka kwa ajili ya mataifa sawasawa na hesabu ya wana wa Israeli. Kwa kuwa fungu la BWANA ni watu wake, Yakobo kura yake ya urithi. Katika nchi ya jangwa alimkuta, katika nyika tupu ivumayo upepo. Alimhifadhi na kumtunza; akamlinda kama mboni ya jicho lake, kama tai avurugaye kiota chake, na kurukaruka juu ya makinda yake, ambaye hutanda mabawa yake kuwadaka, na huwachukua kwenye mabawa yake. BWANA peke yake alimwongoza; hakuwepo mungu mgeni pamoja naye. Akamfanya apande sehemu zilizoinuka za nchi, akamlisha kwa mavuno ya mashamba. Akamlea kwa asali toka mwambani, na kwa mafuta kutoka mwamba mgumu, kwa jibini na maziwa kutoka makundi ya ngʼombe na kutoka makundi ya mbuzi, kwa mafuta ya wana-kondoo na mbuzi, kwa kondoo dume wazuri wa Bashani, na kwa ngano nzuri. Ukanywa damu ya zabibu inayotoa povu.