Kum 29:1-13
Kum 29:1-13 SUV
Haya ndiyo maneno ya agano BWANA alilomwamuru Musa alifanye na wana wa Israeli katika nchi ya Moabu, pamoja na agano alilofanya nao Horebu. Musa akawaita Israeli wote akawaambia, Mmeyaona yote BWANA aliyomfanya Farao katika nchi ya Misri mbele ya macho yenu, yeye na watumwa wake wote, na nchi yake yote; yale majaribu makuu yaliyoyaona macho yako; hizo ishara, na ile miujiza mikuu; lakini BWANA hakuwapa moyo wa kujua, wala macho ya kuona, wala masikio ya kusikia, hata leo hivi. Nami miaka arobaini nimewaongoza jangwani; nguo zenu hazikuchakaa juu yenu, wala kiatu chako hakikuchakaa katika mguu wako. Hamkula mkate, wala hamkunywa divai, wala kileo; ili mpate kujua kwamba Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Nanyi mlipokuja mahali hapa, walitutokea kupigana juu yetu Sihoni mfalme wa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, tukawapiga; tukaitwaa nchi yao, nayo tukawapa Wareubeni, na Wagadi, na nusu ya kabila ya Manase, iwe urithi. Shikeni basi maneno ya agano hili myafanye, ili mfanikiwe katika yote mfanyayo. Leo mmesimama nyote mbele za BWANA, Mungu wenu; wakuu wenu, na kabila zenu, na wazee wenu, na maakida wenu, waume wote wa Israeli, vijana vyenu, na wake wenu, na mgeni wako aliye kati ya kituo chako, tokea mchanjaji wa kuni zako hata mtekaji wa maji yako; ili uingie katika agano la BWANA, Mungu wako, na kiapo chake, afanyacho nawe BWANA, Mungu wako, hivi leo; apate kukuweka leo uwe taifa kwake naye apate kuwa Mungu kwako, kama alivyokuambia, na kama alivyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.