Kumbukumbu la Sheria 29:1-13
Kumbukumbu la Sheria 29:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Haya ni maneno ya agano ambalo Mwenyezi-Mungu aliwaamuru Mose kufanya na Waisraeli katika nchi ya Moabu, licha ya agano Mwenyezi-Mungu alilofanya nao mlimani Horebu. Mose aliwaita pamoja Waisraeli wote akawaambia, “Mliona nyinyi wenyewe jinsi Mwenyezi-Mungu alivyomtendea mfalme wa Misri, maofisa, watumishi wake na nchi yake yote. Mliona maafa makubwa, ishara na maajabu aliyotenda. Lakini mpaka leo Mwenyezi-Mungu hajawapa akili ya kuelewa, macho ya kuona, wala masikio ya kusikia! “Kwa muda wa miaka arubaini, mimi niliwaongoza jangwani, nguo zenu mlizovaa hazikuchakaa wala viatu vyenu havikuchakaa miguuni mwenu. Hamkula mkate wala kunywa divai au kileo chochote kile, mpate kujua kwamba Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu. “Na mlipofika mahali hapa, mfalme Sihoni wa Heshboni na mfalme Ogu wa Bashani walikuja kupigana nasi; lakini tukawashinda, tukaichukua nchi yao, tukayagawia makabila ya Reubeni na Gadi na nusu kabila la Manase iwe mali yao. Kwa hiyo muwe waangalifu kushika maneno yote ya agano hili ili mpate kufanikiwa katika kazi zenu zote. “Leo, mmesimama mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi nyote viongozi wa makabila, wazee wenu, maofisa wenu, watoto wenu na wake zenu, wageni wanaoishi miongoni mwenu ambao hukata kuni na kuwatekea maji. Mko hapa leo ili kufanya agano hili ambalo Bwana Mungu wenu anafanya leo, kwamba atawathibitisha leo kuwa watu wake naye atakuwa Mungu wenu, kama alivyowaapia nyinyi na babu zenu: Abrahamu, Isaka na Yakobo.
Kumbukumbu la Sheria 29:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haya ndiyo maneno ya agano BWANA alilomwamuru Musa alifanye na wana wa Israeli katika nchi ya Moabu, pamoja na agano alilofanya nao Horebu. Musa akawaita Israeli wote akawaambia, Mmeyaona yote BWANA aliyomfanya Farao katika nchi ya Misri mbele ya macho yenu, yeye na watumwa wake wote, na nchi yake yote; yale majaribu makuu yaliyoyaona macho yako; hizo ishara, na ile miujiza mikuu; lakini BWANA hakuwapa moyo wa kujua, wala macho ya kuona, wala masikio ya kusikia, hata leo hivi. Nami miaka arubaini nimewaongoza jangwani; nguo zenu hazikuchakaa juu yenu, wala kiatu chako hakikuchakaa katika mguu wako. Hamkula mkate, wala hamkunywa divai, wala kileo; ili mpate kujua kwamba Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Nanyi mlipokuja mahali hapa, walitutokea kupigana juu yetu Sihoni mfalme wa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, tukawapiga; tukaitwaa nchi yao, nayo tukawapa Wareubeni, na Wagadi, na nusu ya kabila la Manase, iwe urithi. Shikeni basi maneno ya agano hili myafanye, ili mfanikiwe katika yote mfanyayo. Leo mmesimama nyote mbele za BWANA, Mungu wenu; wakuu wenu, na makabila yenu, na wazee wenu, na maofisa wenu, wanaume wote wa Israeli, vijana vyenu, na wake wenu, na mgeni wako aliye kati ya kituo chako, tokea mchanjaji wa kuni zako hata mtekaji wa maji yako; ili uingie katika agano la BWANA, Mungu wako, na kiapo chake, afanyacho nawe BWANA, Mungu wako, hivi leo; apate kukuweka leo uwe taifa kwake naye apate kuwa Mungu kwako, kama alivyokuambia, na kama alivyowaapia baba zako, Abrahamu, na Isaka, na Yakobo.
Kumbukumbu la Sheria 29:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haya ndiyo maneno ya agano BWANA alilomwamuru Musa alifanye na wana wa Israeli katika nchi ya Moabu, pamoja na agano alilofanya nao Horebu. Musa akawaita Israeli wote akawaambia, Mmeyaona yote BWANA aliyomfanya Farao katika nchi ya Misri mbele ya macho yenu, yeye na watumwa wake wote, na nchi yake yote; yale majaribu makuu yaliyoyaona macho yako; hizo ishara, na ile miujiza mikuu; lakini BWANA hakuwapa moyo wa kujua, wala macho ya kuona, wala masikio ya kusikia, hata leo hivi. Nami miaka arobaini nimewaongoza jangwani; nguo zenu hazikuchakaa juu yenu, wala kiatu chako hakikuchakaa katika mguu wako. Hamkula mkate, wala hamkunywa divai, wala kileo; ili mpate kujua kwamba Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Nanyi mlipokuja mahali hapa, walitutokea kupigana juu yetu Sihoni mfalme wa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, tukawapiga; tukaitwaa nchi yao, nayo tukawapa Wareubeni, na Wagadi, na nusu ya kabila ya Manase, iwe urithi. Shikeni basi maneno ya agano hili myafanye, ili mfanikiwe katika yote mfanyayo. Leo mmesimama nyote mbele za BWANA, Mungu wenu; wakuu wenu, na kabila zenu, na wazee wenu, na maakida wenu, waume wote wa Israeli, vijana vyenu, na wake wenu, na mgeni wako aliye kati ya kituo chako, tokea mchanjaji wa kuni zako hata mtekaji wa maji yako; ili uingie katika agano la BWANA, Mungu wako, na kiapo chake, afanyacho nawe BWANA, Mungu wako, hivi leo; apate kukuweka leo uwe taifa kwake naye apate kuwa Mungu kwako, kama alivyokuambia, na kama alivyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.
Kumbukumbu la Sheria 29:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Haya ndiyo maneno ya Agano BWANA aliyomwagiza Mose kufanya na Waisraeli huko Moabu, kuwa nyongeza ya Agano alilofanya nao huko Horebu. Mose akawaita Waisraeli wote akawaambia: Macho yenu yameona yale yote BWANA aliyofanya kwa Mfalme Farao huko Misri, kwa maafisa wake wote na kwa nchi yake yote. Kwa macho yenu wenyewe mliona yale majaribu makubwa, ishara zile za miujiza na maajabu makubwa. Lakini mpaka leo BWANA hajawapa akili ya kuelewa au macho yanayoona au masikio yanayosikia. Kwa muda wa miaka arobaini niliyowaongoza jangwani, nguo zenu hazikuchakaa, wala viatu miguuni mwenu. Hamkula mkate na hamkunywa divai wala kileo chochote. Nilifanya hivi ili mpate kujua kuwa mimi ndimi BWANA Mungu wenu. Wakati mlipofika mahali hapa, Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani walikuja kupigana dhidi yetu, lakini tuliwashinda. Tuliichukua nchi yao na kuwapa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kama urithi wao. Fuateni kwa bidii masharti ya Agano hili, ili kwamba mweze kustawi katika kila kitu mnachofanya. Ninyi nyote leo mnasimama mbele za BWANA Mungu wenu; mkiwa viongozi na wakuu wenu, wazee na maafisa wenu, na wanaume wengine wote wa Israeli, pamoja na watoto wenu, wake zenu na pia wageni waishio katika kambi zenu wanaowapasulia kuni na kuwachotea maji. Mnasimama hapa ili kufanya Agano na BWANA Mungu wenu, Agano ambalo Mungu analifanya nanyi siku hii ya leo na kulitia muhuri kwa kiapo, kuwathibitisha ninyi siku hii ya leo kama taifa lake, ili aweze kuwa Mungu wenu kama alivyowaahidi na kama alivyowaapia baba zenu Abrahamu, Isaki na Yakobo.