2 Sam 6:11-23
2 Sam 6:11-23 SUV
Sanduku la BWANA akalitia katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye BWANA akambarikia Obed-edomu, na nyumba yake yote. Kisha mfalme Daudi akaambiwa ya kwamba, BWANA ameibarikia nyumba ya Obed-edomu, na vitu vyote alivyo navyo kwa ajili ya sanduku la Mungu. Daudi akaenda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe. Hata ikawa, watu waliolichukua sanduku la BWANA walipokwisha kwenda hatua sita, akachinja ng’ombe na kinono. Daudi akacheza mbele za BWANA kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani. Basi Daudi na nyumba yote ya Israeli wakalileta sanduku la BWANA kwa shangwe, na kwa sauti ya tarumbeta. Ikawa, sanduku la BWANA lilipoingia mji wa Daudi Mikali, binti Sauli, akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi akiruka-ruka na kucheza mbele za BWANA; akamdharau moyoni mwake. Wakaliingiza sanduku la BWANA, na kuliweka mahali pake, katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za BWANA. Kisha Daudi alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani akawabarikia watu kwa jina la BWANA wa majeshi. Akawagawia watu wote, mkutano wote wa Israeli, wanaume kwa wanawake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu. Basi watu wote wakaenda zao, kila mtu nyumbani kwake. Ndipo Daudi akarudi ili awabarikie watu wa nyumbani mwake. Na Mikali, binti Sauli, akatoka nje aende kumlaki Daudi, naye akasema, Mfalme wa Israeli alikuwa mtukufu leo namna gani, akijifunua mwili wake mbele ya vijakazi vya watumishi wake, mfano wa watu baradhuli mmojawapo, ajifunuavyo mwili wake mbele ya watu, asipokuwa na haya! Daudi akamwambia Mikali, Ilikuwa mbele za BWANA, aliyenichagua mimi juu ya baba yako, na juu ya nyumba yake, ili kuniweka niwe mkuu juu ya watu wa BWANA, juu ya Israeli; kwa hiyo mimi nitacheza mbele za BWANA. Kisha nitakuwa hafifu zaidi, nami nitakuwa mnyonge machoni pangu mimi mwenyewe; lakini kwa wale vijakazi uliowanena, kwao nitaheshimiwa. Basi Mikali, binti Sauli, hakuwa na mtoto hata siku ya kufa kwake.