Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 6:11-23

2 Samweli 6:11-23 NENO

Sanduku la Mwenyezi Mungu likakaa katika nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti, kwa miezi mitatu, naye Mwenyezi Mungu akambariki pamoja na nyumba yake yote. Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, “Mwenyezi Mungu ameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu.” Basi Daudi akateremka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu hadi Mji wa Daudi kwa shangwe. Wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Mwenyezi Mungu walipotembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenoneshwa. Daudi, akiwa amevaa kizibau cha kitani, alicheza mbele za Mwenyezi Mungu kwa nguvu zake zote, wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu kwa shangwe na sauti za tarumbeta. Sanduku la Mwenyezi Mungu lilipokuwa linaingia Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele za Mwenyezi Mungu, akamdharau moyoni mwake. Wakaleta Sanduku la Mwenyezi Mungu na kuliweka mahali pake ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mwenyezi Mungu. Baada ya kumaliza kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, Daudi akawabariki watu katika jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Kisha akatoa mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu kwa kila mtu katika mkutano wote wa Waisraeli, wanaume kwa wanawake. Nao watu wote wakaenda nyumbani. Daudi aliporudi ili kuwabariki watu wa nyumbani mwake, Mikali binti Sauli akatoka nje kumlaki, akamwambia, “Tazama jinsi mfalme wa Israeli alivyojibainisha mwenyewe leo kwa kuvua mavazi yake machoni pa vijakazi wa watumishi wake, vile mtu asiye na adabu angefanya!” Daudi akamwambia Mikali, “Nilifanya hivyo mbele za Mwenyezi Mungu ambaye alinichagua mimi badala ya baba yako au mwingine yeyote kutoka nyumba yake aliponiweka niwe mtawala wa Israeli, watu wa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo nitacheza mbele za Mwenyezi Mungu. Nitakuwa asiye na heshima kuliko sasa, nami nitajishusha machoni pangu mwenyewe. Lakini kwa hawa vijakazi uliosema habari zao nitaheshimiwa.” Naye Mikali binti Sauli hakuwa na watoto hadi siku ya kufa kwake.