2 Sam 5:17-25
2 Sam 5:17-25 SUV
Na hao Wafilisti waliposikia kwamba wamemtia Daudi mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akapata habari, akashuka akaenda ngomeni. Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya bondeni mwa Warefai. Basi Daudi akauliza kwa BWANA, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti? Utawatia mkononi mwangu? Naye BWANA akamwambia Daudi, Panda; kwa kuwa hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako. Basi Daudi akaja Baal-perasimu, naye Daudi akawapiga huko; akasema, BWANA amewafurikia adui zangu mbele yangu, kama mafuriko ya maji. Basi akapaita mahali pale Baal-perasimu. Nao wakaziacha sanamu zao huko, na Daudi na watu wake wakaziondolea mbali. Lakini wakapanda hao Wafilisti tena mara ya pili, wakajitawanya bondeni mwa Warefai. Naye Daudi alipouliza kwa BWANA, alisema, Usipande; zunguka nyuma yao, ukawajie huko mbele ya miforsadi. Kisha itakuwa, hapo utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo nawe ujitahidi; kwa maana ndipo BWANA ametoka mbele yako awapige jeshi la Wafilisti. Ndivyo alivyotenda Daudi, vile vile kama BWANA alivyomwagiza; naye akawapiga Wafilisti toka Geba hata ujapo Gezeri.