2 Samweli 5:17-25
2 Samweli 5:17-25 NENO
Wafilisti waliposikia kuwa Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akateremka kwenye ngome. Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kusambaa kwenye Bonde la Warefai, kwa hiyo Daudi akamuuliza Mwenyezi Mungu, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nenda, kwa maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.” Ndipo Daudi akaenda Baal-Perasimu, na huko akawashinda Wafilisti. Akasema, “Kama mafuriko yanavyofurika, Mwenyezi Mungu amewafurikia adui zangu mbele yangu.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-Perasimu. Wafilisti wakaziacha sanamu zao huko, naye Daudi na watu wake wakazichukua. Wafilisti walikwea kwa mara nyingine na kusambaa katika Bonde la Warefai. Kwa hiyo Daudi akamuuliza Mwenyezi Mungu, naye akamjibu, “Usipande moja kwa moja, bali wazungukie kwa nyuma na uwashambulie mbele ya miti ya miforosadi. Mara utakaposikia sauti ya kutembea kwenye vilele vya miti ya miforosadi, nenda haraka, kwa sababu hiyo itamaanisha kuwa Mwenyezi Mungu ametangulia mbele yako kupiga jeshi la Wafilisti.” Basi Daudi akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza, naye akawaangusha Wafilisti njia yote kuanzia Geba hadi Gezeri.