2 Sam 11:14-27
2 Sam 11:14-27 SUV
Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria. Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe. Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa. Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa. Ndipo Yoabu akapeleka na kumwarifu Daudi habari zote za vita; akamwagiza yule mjumbe, akisema, Ukiisha kumpa mfalme habari zote za vita, itakuwa, hasira ya mfalme ikiwaka, akakuambia, Kwani mliukaribia mji namna ile ili kuupiga? Je! Hamkujua ya kuwa watapiga mishale toka ukutani? Ni nani aliyempiga Ahimeleki, mwana wa Yeru-beshethi? Je! Si mwanamke aliyemtupia jiwe la kusagia la juu kutoka ukutani? Hata akafa huko Thebesi? Kwani kuukaribia ukuta namna ile? Ndipo utakaposema, Mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa naye. Basi yule mjumbe akaenda, akafika na kumwonyesha Daudi yote aliyomtuma Yoabu. Yule mjumbe akamwambia Daudi, Watu hao walitushinda, wakatutokea nje hata uwandani, tukashindana nao hata mahali pa kuingilia langoni. Wapiga mishale wakatupiga sisi, watumishi wako, toka juu ya ukuta; na baadhi ya watumishi wa mfalme wamekufa, na Uria, Mhiti, mtumishi wako, amekufa naye. Basi Daudi akamwambia yule mjumbe, Basi, mwambie Yoabu maneno haya, Jambo hili lisiwe baya machoni pako, maana upanga hula huyu kama unavyomla huyu; zidi kutia nguvu vita vyako juu ya mji ukauangushe; nawe mtie moyo. Na yule mke wa Uria alipopata habari ya kuwa Uria mumewe amekufa, akamwombolezea mumewe. Hata maombolezo hayo yalipokwisha, Daudi akatuma mtu, akamtwaa, akamtia nyumbani mwake; naye akawa mkewe, akamzalia mwana.