2 Samueli 11:14-27
2 Samueli 11:14-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Asubuhi yake, Daudi alimwandikia Yoabu barua akampa Uria aipeleke kwa Yoabu. Katika barua hiyo Daudi aliandika hivi: “Mweke Uria kwenye mstari wa mbele, mahali ambako mapigano ni makali kabisa, kisha umwache huko na kurudi nyuma ili apigwe, afe.” Basi, Yoabu alipokuwa anauzingira mji alimweka Uria mahali ambapo alijua wazi wanajeshi wa adui walikuwa hodari sana. Wakazi wa mji huo walitoka katika mji wao na kupigana na Yoabu. Baadhi ya watumishi wa Daudi, waliuawa. Uria Mhiti naye aliuawa pia. Kisha, Yoabu alipeleka habari zote kwa Daudi akimweleza juu ya vita. Yoabu akamwamuru huyo mtumishi aliyemtuma hivi, “Baada ya kumweleza mfalme mambo yote kuhusu vita, akikasirika na kukuuliza, ‘Kwa nini mlikwenda karibu na mji mlipokuwa mnapigana? Hamkujua kwamba wangewapiga mishale kutoka kwenye kuta za mji wao? Nani alimuua Abimeleki mwana wa Yerubeshethi? Si alikuwa mwanamke mmoja mjini Thebesi ambaye alitupa jiwe la kusagia kutoka kwenye ukuta nalo likamuua Abimeleki? Kwa nini basi, mlikwenda karibu na ukuta?’ Basi, wewe utamwambia hivi, ‘Hata mtumishi wako Uria Mhiti, naye amekufa.’” Yule mjumbe alikwenda kwa Daudi na kumwambia yote aliyotumwa na Yoabu ayaseme. Yule mjumbe akamwambia Daudi, “Adui zetu walituzidi nguvu, wakatoka nje ya miji na kutushambulia nyikani. Hata hivyo sisi tuliwarudisha mpaka kwenye lango la mji. Halafu wakatupiga mishale sisi watumishi wako kutoka ukutani. Baadhi ya watumishi wako waliuawa. Hata mtumishi wako Uria, Mhiti, naye amekufa.” Daudi akamwambia yule mjumbe, “Utamwambia hivi Yoabu, ‘Jambo hili lisikusumbue kwani upanga hauna macho, vita huua yeyote yule. Bali, imarisha mashambulizi dhidi ya mji, hadi umeuangamiza mji huo’. Ndivyo utakavyomtia moyo Yoabu.” Bathsheba mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe Uria amekufa, alimwombolezea mumewe. Muda wa matanga ulipokwisha, Daudi aliagiza Bathsheba achukuliwe na kupelekwa nyumbani kwake. Bathsheba akawa mke wa Daudi, naye akamzalia Daudi mtoto wa kiume. Lakini jambo hilo alilofanya Daudi lilimchukiza Mwenyezi-Mungu.
2 Samueli 11:14-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu barua, akaituma kwa mkono wa Uria. Akaandika katika barua hiyo, akasema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe. Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa. Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria, Mhiti, naye akafa. Ndipo Yoabu akapeleka ujumbe na kumwarifu Daudi habari zote za vita; akamwagiza yule mjumbe, akisema, Ukiisha kumpa mfalme habari zote za vita, kisha, ikiwa hasira ya mfalme itawaka, akakuambia, Kwa nini mliukaribia mji namna ile ili kuupiga? Je! Hamkujua ya kuwa watapiga mishale toka ukutani? Ni nani aliyempiga Ahimeleki, mwana wa Yeru-beshethi? Je! Si mwanamke aliyemtupia jiwe la kusagia la juu kutoka ukutani? Hata akafa huko Thebesi? Kwa nini mliukaribia ukuta namna ile? Ndipo utakaposema, Mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa naye. Basi yule mjumbe akaenda, akafika na kumwonesha Daudi yote aliyomtuma Yoabu. Yule mjumbe akamwambia Daudi, Watu hao walitushinda, wakatutokea nje hata uwandani, tukashindana nao hadi mahali pa kuingilia langoni. Wapiga mishale wakatupiga sisi, watumishi wako, toka juu ya ukuta; na baadhi ya watumishi wa mfalme wamekufa, na Uria, Mhiti, mtumishi wako, amekufa naye. Basi Daudi akamwambia yule mjumbe, Basi, mwambie Yoabu maneno haya, Jambo hili lisiwe baya machoni pako, maana upanga hula huyu kama unavyomla huyu; zidi kutia nguvu vita vyako juu ya mji ukauangushe; nawe mtie moyo. Na yule mke wa Uria alipopata habari ya kuwa Uria mumewe amekufa, akamwombolezea mumewe. Hata maombolezo hayo yalipokwisha, Daudi akatuma mtu, akamtwaa, akamtia nyumbani mwake; naye akawa mkewe, akamzalia mtoto wa kiume.
2 Samueli 11:14-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria. Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe. Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa. Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa. Ndipo Yoabu akapeleka na kumwarifu Daudi habari zote za vita; akamwagiza yule mjumbe, akisema, Ukiisha kumpa mfalme habari zote za vita, itakuwa, hasira ya mfalme ikiwaka, akakuambia, Kwani mliukaribia mji namna ile ili kuupiga? Je! Hamkujua ya kuwa watapiga mishale toka ukutani? Ni nani aliyempiga Ahimeleki, mwana wa Yeru-beshethi? Je! Si mwanamke aliyemtupia jiwe la kusagia la juu kutoka ukutani? Hata akafa huko Thebesi? Kwani kuukaribia ukuta namna ile? Ndipo utakaposema, Mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa naye. Basi yule mjumbe akaenda, akafika na kumwonyesha Daudi yote aliyomtuma Yoabu. Yule mjumbe akamwambia Daudi, Watu hao walitushinda, wakatutokea nje hata uwandani, tukashindana nao hata mahali pa kuingilia langoni. Wapiga mishale wakatupiga sisi, watumishi wako, toka juu ya ukuta; na baadhi ya watumishi wa mfalme wamekufa, na Uria, Mhiti, mtumishi wako, amekufa naye. Basi Daudi akamwambia yule mjumbe, Basi, mwambie Yoabu maneno haya, Jambo hili lisiwe baya machoni pako, maana upanga hula huyu kama unavyomla huyu; zidi kutia nguvu vita vyako juu ya mji ukauangushe; nawe mtie moyo. Na yule mke wa Uria alipopata habari ya kuwa Uria mumewe amekufa, akamwombolezea mumewe. Hata maombolezo hayo yalipokwisha, Daudi akatuma mtu, akamtwaa, akamtia nyumbani mwake; naye akawa mkewe, akamzalia mwana.
2 Samueli 11:14-27 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kesho yake asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu barua, akamtuma Uria kuipeleka. Ndani ya barua aliandika, “Mweke Uria mstari wa mbele ambapo mapigano ni makali sana. Kisha wewe uondoke ili Uria aangushwe chini na kuuawa.” Hivyo Yoabu alipokuwa ameuzingira mji kwa jeshi, akamweka Uria mahali alipojua kuwa ulinzi wa adui ulikuwa imara sana. Wanaume wa mji walipotoka kwenda kupigana dhidi ya Yoabu, baadhi ya watu katika jeshi la Daudi wakauawa; zaidi ya hayo, Uria Mhiti akafa. Yoabu akampelekea Daudi maelezo yote ya vita. Akamwagiza mjumbe hivi, “Utakapokuwa umemaliza kumpa mfalme maelezo ya vita, hasira ya mfalme yaweza kuwaka, naye aweza kukuuliza, ‘Kwa nini mlisogea karibu hivyo na mji kupigana? Hamkujua kuwa wangeweza kuwapiga mishale kutoka ukutani? Ni nani aliyemuua Abimeleki mwana wa Yerub-Besheth? Je, mwanamke hakutupa juu yake jiwe la juu la kusagia kutoka ukutani, kwa hiyo akafa huko Thebesi? Kwa nini mlisogea hivyo karibu ya ukuta?’ Akikuuliza hivi, ndipo umwambie, ‘Pia mtumishi wako Uria Mhiti amekufa.’ ” Mjumbe akaondoka. Alipowasili akamwambia Daudi kila kitu alichokuwa ametumwa na Yoabu kusema. Mjumbe akamwambia Daudi, “Watu walituzidi nguvu wakatoka nje ya mji dhidi yetu kwenye eneo la wazi, lakini tuliwarudisha nyuma hadi ingilio la mji. Ndipo wapiga upinde walitupa mishale kwa watumishi wako kutoka ukutani, na baadhi ya watu wa mfalme wakafa. Zaidi ya hayo, Uria Mhiti, mtumishi wako, amekufa.” Daudi akamwambia mjumbe, “Ukamwambie Yoabu hivi, ‘Jambo hili lisikutie wasiwasi, upanga hula huyu sawa na ulavyo mwingine. Zidisha mashambulizi dhidi ya mji na uangamize.’ Mwambie Yoabu hivi ili kumtia moyo.” Mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe amekufa, akamwombolezea. Baada ya muda wa maombolezo kwisha, Daudi akatumana aletwe nyumbani mwake. Naye akawa mkewe, na akamzalia mwana. Lakini jambo alilofanya Daudi lilimchukiza Mwenyezi Mungu.