2 Samweli 11:14-27
2 Samweli 11:14-27 NENO
Kesho yake asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu barua, akamtuma Uria kuipeleka. Ndani ya barua aliandika, “Mweke Uria mstari wa mbele ambapo mapigano ni makali sana. Kisha wewe uondoke ili Uria aangushwe chini na kuuawa.” Hivyo Yoabu alipokuwa ameuzingira mji kwa jeshi, akamweka Uria mahali alipojua kuwa ulinzi wa adui ulikuwa imara sana. Wanaume wa mji walipotoka kwenda kupigana dhidi ya Yoabu, baadhi ya watu katika jeshi la Daudi wakauawa; zaidi ya hayo, Uria Mhiti akafa. Yoabu akampelekea Daudi maelezo yote ya vita. Akamwagiza mjumbe hivi, “Utakapokuwa umemaliza kumpa mfalme maelezo ya vita, hasira ya mfalme yaweza kuwaka, naye aweza kukuuliza, ‘Kwa nini mlisogea karibu hivyo na mji kupigana? Hamkujua kuwa wangeweza kuwapiga mishale kutoka ukutani? Ni nani aliyemuua Abimeleki mwana wa Yerub-Besheth? Je, mwanamke hakutupa juu yake jiwe la juu la kusagia kutoka ukutani, kwa hiyo akafa huko Thebesi? Kwa nini mlisogea hivyo karibu ya ukuta?’ Akikuuliza hivi, ndipo umwambie, ‘Pia mtumishi wako Uria Mhiti amekufa.’ ” Mjumbe akaondoka. Alipowasili akamwambia Daudi kila kitu alichokuwa ametumwa na Yoabu kusema. Mjumbe akamwambia Daudi, “Watu walituzidi nguvu wakatoka nje ya mji dhidi yetu kwenye eneo la wazi, lakini tuliwarudisha nyuma hadi ingilio la mji. Ndipo wapiga upinde walitupa mishale kwa watumishi wako kutoka ukutani, na baadhi ya watu wa mfalme wakafa. Zaidi ya hayo, Uria Mhiti, mtumishi wako, amekufa.” Daudi akamwambia mjumbe, “Ukamwambie Yoabu hivi, ‘Jambo hili lisikutie wasiwasi, upanga hula huyu sawa na ulavyo mwingine. Zidisha mashambulizi dhidi ya mji na uangamize.’ Mwambie Yoabu hivi ili kumtia moyo.” Mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe amekufa, akamwombolezea. Baada ya muda wa maombolezo kwisha, Daudi akatumana aletwe nyumbani mwake. Naye akawa mkewe, na akamzalia mwana. Lakini jambo alilofanya Daudi lilimchukiza Mwenyezi Mungu.